Na RAPHAEL OKELLO,
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Janet Mayanja ameiomba Wizara ya Maliasili na utalii kuangalia uwezekano wa kuwadhibiti tembo kutoka ndani ya Hifadhi Taifa ya Serengeti.
Amesema wanyama hao wamekuwa wakiharibu mali za wananchi ndani ya mji wa Bunda.
Mayanja alisema hivi sasa wimbi la tembo kutoka katika hifadhi hiyo na kuvamia makazi ya watu limekuwa kubwa na kuongezeka kwa kasi.
Alisema  Wizara ya Maliasili inapaswa kufikiri kwa kina au kufanya utafiti wa nini kifanyike ili kutatua jambo hilo.
“Ni kweli tembo hawa wanaharibu mali za wananchi lakini mbaya zaidi  wananchi wale ambao bado wanategemea kilimo pembezoni mwa mji, mazao yao yanaharibika   na kuwasababishia baa la njaa.
“Tunaiomba Wizara ya Maliasili kuangalia ni namna gani tembo hawa wanaweza kudhibitiwa, sisi kama halmashauri tunafanya kila tunaloweza katika kukabiliana na janga hili lakini nguvu yetu ni ndogo.
Katika siku za hivi karibuni makundi  ya tembo yaliwavamia makazi ya wananchi  wa vijiji vya Nyatare, Kunzugu, Tamao na Nyatware, katika halmashauri ya mji huo  kuvunja ghala na kula mazao ya akiba yaliyohifadhiwa na wananchi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Charles Mlingwa alisema  serikali inalifanyia kazi tatizo hilo la tembo na wanyama pori wengine wanaofanya uharibifu.