Na MANENO SELANYIKA –DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es Salaam imempa dhamana Mtafiti wa masuala ya Afya, Glory Anthony (36),anayetuhumiwa kumuua bila kukusudia rafiki yake, Josephat Mwakitwange.
Mahakama hiyo jana ilikubali maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi.
Uamuzi huo ulitolewa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Issa Kasailo.
Upande wa Jamhuri ulikuwa unasimamiwa na Wakili wa Serikali, Matarasa Maharagande wakati upande wa utetezi uliongozwa na mawakili wawili, Godluck Walter na Abdullah Lyana.
Wakili wa Serikali, Matarasa alidai kuwa shauri hilo lipo mbele ya mahakama hiyo kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo wa dhamana uliowasilishwa na upande wa utetezi.
Wakili Walter aliiambia mahakama hiyo kuwa kulingana na kosa la mteja wake, anaomba apatiwe dhamana kwa sababu mahakama hiyo ina uwezo huo.
Alisema Jaji Fauz Twaib wa mahakama kuu kupitia kesi namba 46\ 2012 iliyokuwa inamkabili Elizabeth Michael maarufu Lulu alidhaminiwa.
“Katika kesi hiyo Jaji Twaib alisisitiza kwamba si lazima mahakama kuu itoe uamuzi wa dhamana bali hata za chini zina uwezo wa kutoa dhamana katika kesi ya mauaji bila kukusudia, akitoa mfano wa kesi ya Lulu iliyotolewa uamuzi wa dhamana Juni 11,2011 ,” alidai Wakili Walter.