25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

AMWACHA MUMEWE ILI AOLEWE NA MGANGA MWENYE WAKE 8

MWANAMUME wa miaka 45 aliyeachwa na mke aliyeenda kuolewa kama mke wa tisa na mganga wa kienyeji, sasa atarejeshewa mahari na gharama ya kumsomesha mtalaka wake huyo.

Mwanaume huyo, James Mayaka alikuwa na furaha tele baada ya Mahakama ya Rufaa mjini Kisumu kuamuru arejeshewe Sh 200,000 za Kenya sawa na Sh milioni nne za Tanzania.

Alisema hatimaye amepata haki yake baada ya kesi kuunguruma kwa miaka sita mahakamani.

Kati ya fedha anazotarajia kupata ni pamoja na zile alizotumia kumsomesha mkewe huyo wa zamani Everline Kerubo Makini katika Chuo cha Ualimu cha Narok kati ya mwaka 2002 na 2004.

Awali mkewe huyo alikuwa amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kisii uliotolewa Februari 2015.

Lakini majaji wa Mahakama ya Rufaa Wanjiru Karanja, Festus Azangalala na Gatembu Kairu, walisema kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa sahihi.

Mahakama ya Kisii ilikuwa imeamuru Makini, arejeshe Sh 205,000 za Kenya kama sehemu ya malipo ya mahari na karo ya chuo pamoja na riba.

Mayaka ambaye ni naibu wa mwalimu mkuu wa shule moja ya sekondari alikuwa ameiomba mahakama hiyo ya Kisii imwamuru Kerubo amrejeshee Sh 209,000 ambazo alikuwa amemlipia kama karo ya chuo.

Pia alitaka mahakama kumshurutisha mkewe huyo wa zamani amrejeshee Sh 120,000 alizolipa kama mahari.

Hata hivyo, mahakama iliamuru Kerubo arejeshe kiwango nusu kwa kila suala yaani Sh104,000 kwa karo na Sh60,000 kwa mahari. Jumla ilikuwa ni Sh164,000 za Kenya.

Kiwango hicho hata hivyo kiliongezeka na kufikia 205,000 baada ya riba kujumuishwa.  Uamuzi huo ulisomwa na Jaji Chrispin Nangila kwa niaba ya Jaji Ruth Sitati Februari 27, 2015.

Anaongeza kuwa bado anafuatilia kesi katika Mahakama ya Nyamira inayolenga kumwezesha kuishi na watoto wake, ambao wana umri wa miaka 13 na 11.

“Aliwachukua watoto wetu kwa nguvu, hivyo nataka nirejeshewe kisheria kwani najua wanataabika,” anasema.

Anasema Kerubo huwabadilishia makao mara kwa mara kwa jamaa zake kwa sababu anazozielewa yeye.

Wawili hao walitengana mwaka 2009 baada ya mke kuamua kwenda kuolewa na mganga wa kienyeji ambaye tayari alikuwa na wake 8, yeye akiwa wa tisa.

Walioana ndoa ya kimila za utamaduni wa Wakisii mwaka 2000. Walifunga ndoa rasmi mwaka wa 2004 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamira.

Mayaka anasema mke huyo wa umri wa miaka 42 alimkimbia na kwenda kuolewa na mganga mmoja katika eneo la Daraja Mbili mjini Kisii kuwa mke wa tisa wa mganga huyo.

Anasema wanaume wengi huogopa kutafuta haki wanapokandamizwa katika ndoa wakihofia kuonekana wanyonge.

“Wengine hawana ufahamu kuwa wanaweza kutafuta haki,” anasema Mayaka, ambaye yupo tayari kuoa mke mwingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles