33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HAPI NA MPANGO WA KUJENGA SHULE ZA KISASA

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni ina ukubwa wa kilomita za mraba 320.

Wilaya hiyo imepakana na Wilaya ya Bagamoyo upande wa Kaskazini, upande wa Kaskazini Mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini inapakana na Manispaa ya Ilala, upande wa Kusini Magharibi inapakana na Wilaya ya Kisarawe na upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Ubungo.

Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, yanaonyesha kuwa Kinondoni ina idadi ya watu 1,775,049, kati ya hao wanaume ni  860,802 na wanawake 914,247 huku  ikiwa na ongezeko la watu kwa wastani wa asilimia tano.

Kinondoni imegawanyika katika tarafa mbili, kata 20, jumla ya mitaa 112 na majimbo mawili ambayo ni Kawe na Kinondoni.

Wananchi wa manispaa hiyo wanategemea biashara kubwa na ndogo, ufugaji, kilimo na bustani, viwanda vikubwa na vidogo na utalii.

 

AJIRA

Wananchi wa Kinondoni wameajiriwa katika sekta rasmi na wengine katika sekta zisizo la rasmi.

 

ELIMU YA MSINGI

 

Kumekuwa na ongezeko katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza tangu Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulipoanza nchini mwaka 2002. Hii imetokana na kuhamasika kwa jamii katika suala zima la kuandikisha watoto kuanza shule, pia kuongezeka kwa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na upatikanaji wa miundombinu mingine ya vyoo, madawati, walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. 

 

ELIMU YA SEKONDARI

Kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari kwa sababu ya sera ya elimu bure.

 

AFYA

Wilaya hiyo imeendelea kutoa huduma za afya kupitia Hospitali ya Mwananyamala, vituo vya afya na zahanati ambapo huduma zinazotolewa ni magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, pamoja na kinga za magonjwa mbalimbali.

 

 MALIASILI NA UVUVI

Halmashauri inaendelea kutunza miti na kuhifadhi mazingira kwa kuotesha miti mbalimbali.

Aidha mradi wa Uwiano na Usimamizi wa Mazingira ya Pwani (KICAMP) unasimamia na kutunza rasilimali za fukwe na bahari katika maeneo ya Msasani, Kunduchi, Ununio na Mbweni.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ni mmoja wa viongozi ambao wamedhamiria kwa dhati kubadili taswira ya wananchi wa wilaya hiyo kwa kuboresha maeneo muhimu kama sekta ya elimu, biashara, uvuvi na kulinda maeneo ya wazi yasiendelee kuporwa na wajanja wachache.

Hapi anasema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uhaba wa viwanja vya umma jambo ambalo linachangia baadhi ya maeneo kushindwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa sababu ya kukosa viwanja.

Anasema uzembe wa baadhi ya viongozi waliopita wamechangia kwa kiasi fulani maeneo ya wazi kuporwa au kuuzwa kinyemela kwa wajanja.

Anaongeza kuwa mbali ya changamoto wanazokabiliana nazo, anafanya jitihada za kuanzisha kampeni maalumu ya kurejesha viwanja vyote vya umma vilivyouzwa bila kufuata utaratibu.

"Katika hili hatutakuwa na huruma bila kujali cheo, au umenunua shilingi ngapi tutahakikisha kila aliyejimilikisha au kuuziwa kiwanja cha serikali anakirejesha iwezekanavyo," anasema Hapi.

 

Hapi anawataka wananchi waliojimilikisha maeneo hayo waanze kujisalimisha wenyewe kabla hawajakumbwa na mkono wa sheria.

Anasema urejeshwaji wa maeneio hayo hata kama yamejengwa utasaidia kujenga majengo muhimu ikiwamo masoko, shule na vituo vya afya.

 

MIGOGORO 

Hapi anasema kuanzia sasa ameamua kuunda utaratibu mpya ambao utasaidia kupunguza migogoro kwenye masoko ambapo wakusanyaji wa ushuru watakuwa ni mameneja.

"Nimejifunza mambo mengi migogoro mingi katika masoko hutokana na uchu wa madaraka na kujilimbikizia fedha…kwani manispaa ilikuwa inapata fedha kidogo, nyingi zinaliwa na wajanja," anasema Hapi.

Anasema ana mifano ya kutosha katika soko la Makumbusho, mapato kwa mwezi ilikuwa ni Sh milioni mbili lakini kwa sasa imefika Sh milioni nane baada ya kupeleka meneja aliyeajiriwa na serikali.

 

ARDHI

Hapi anasema manispaa hiyo imesikiliza na kutoa uamuzi wa mashauri zaidi ya 1,000 yanayohusu migogoro ya ardhi ndani ya manispaa hiyo.

Anasema wilaya hiyo inasifika kwa migogoro ya ardhi lakini kwa sasa ameamua kuunda timu ya kuchunguza migogoro pamoja na kupimwa viwanja na mashamba katika manispaa hiyo ili kutoa hati zikazopunguza kero za uvamizi wa maeneo hayo.

 

MATARAJIO

Hapi anasema anatarajia kuibadili Kinondoni kuwa ya kisasa zaidi ambapo amewaagiza maofisa ardhi kununua ramani za mipango miji na kuzigawa kwa watendaji wa kata ili kila mmoja aelewe mipaka na uhalali wa maeneo mbalimbali.

Pia anasema wana mikakati madhubuti ya ujenzi wa dampo la kisasa ambalo litasaidia kupunguza adha ya kutupa taka ovyo au kwenda Pugu Kajiungeni ambako manispaa inatumia gharama kubwa kusafirisha takataka.

Anaongeza kuwa ni vyema watendaji wa manispaa hiyo kujenga mazingira mazuri ya elimu kwa wanafunzi kwa kujenga shule za kisasa, miundombinu pamoja na uzio ili kuleta hamasa ya wanafunzi kufaului vizuri.

"Katika hili naagiza ofisa elimu ahakikishe walimu wanatosha katika shule zetu, kujenga miundombinu bora ili kuleta hamasa za wanafunzi kujisomea kwa bidii…mbali ya changamoto tuliyonayo hivi sasa ya mfumuko wa wanafunzi katika shule zetu za sekondari ambao umekuja kwa sababu ya elimu bure kwani hivi sasa asilimia 90 ya wanafunzi wamejiunga na shule hasa za kata," anasema Hapi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles