Na PENDO FUNDISHA – MBEYA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, linamshikilia mchimba dhahabu, Shija Salum (38), mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kumuua rafiki yake na kula ubongo wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba pamoja na mtuhumiwa huyo kula ubongo wa rafiki yake huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Shija, pia alitafuna sehemu zake za siri baada ya kuzikata.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, usiku katika Kijiji cha Manyanya, Kata ya Makongorosi, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Alisema mtuhumiwa na marehemu walifika kijijini hapo wakitokea Shinyanga miezi mitatu iliyopita.
“Inasemekana wawili hao walikuwa ni marafiki kwani walifika wilayani Chunya, Kata ya Makongolosi kwenye machimbo ya dhahabu yanayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja aitwaye Teddy Mwantega.
“Siku hiyo ya tukio, marehemu Shija, alikuwa amejilaza mahali na hapo ndipo alipofika rafiki yake huyo, akiwa na panga mkononi na kumkata kwa nguvu kichwani.
“Baada ya hapo, alimvua nguo na kuzikata sehemu zake za siri na kuzishika mkononi.
“Wakati akiwa na sehemu hizo za siri mkononi, alichukua ubongo wa marehemu na kuula, kisha akatafuna zile sehemu za siri.
“Kwahiyo, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika,” alisema Kamanda Kidavashari.
Wakati huo huo, Upendo Mosha anaripoti kutoka Moshi, kwamba watu watatu wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro katika matukio mawili tofauti, likiwamo la wanafunzi wawili kufa maji wakati wakiogelea katika Ziwa Chala, lililoko wilayani Rombo.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema tukio la wanafunzi lilitokea Desemba 26, mwaka huu, saa 10 jioni.
Alisema wanafunzi hao ambao ni wa kidato cha nne na pili katika shule mbili tofauti walifia katika ziwa hilo wakati walipokuwa wakiogelea.
Aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Joseph Maranya (18) wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Serengeti, mkoani Mara na Mogesa Chacha (17), mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwika wilayani Moshi.
“Baada ya wanafunzi hao kuzama, jitihada za kuwaokoa zilifanyika bila mafanikio na Desemba 27, mwaka huu, polisi kwa kushirikiana na kikosi cha zimamoto na uokoaji, walishirikiana kuopoa miili ya marehemu.
“Hata hivyo, tulifanikiwa kuupata mwili wa Joseph, lakini bado tunaendelea kuutafuta mwili wa mwanafunzi Mogesa,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Katika tukio jingine, mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Judica Simoni mwenye umri wa miaka kati ya 30 na 35, mkazi wa Machame, Wilaya ya Hai mkoani hapa, alishambuliwa na kuuawa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi.
Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Desemba 26, mwaka huu, saa 11 jioni, katika Kijiji cha Narumu Ushari, wilayani humo.
“Kutokana na tukio hilo, wanaoshikiliwa ni Asanterabi Mbowe (47), Nimrod Mbowe na Cathbeth Jacob (28).
“Kwahiyo, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa uchunguzi,” alisema Kamanda Mutafungwa.