24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WADAIWA BODI YA MIKOPO KUSAKWA MAJUMBANI USIKU

*Kutafutwa kumbi za starehe, nyumba za ibada

*Wanaosoma nchini China kukosa mikopo


 

abdul-razaq-badruNa CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema kuanzia Januari mwakani itaanza kudai fedha za mikopo kwa kupita nyumba kwa nyumba, hasa muda wa usiku.

Mbali na hilo, HESLB wamesema kuwa wapo kwenye mpango wa kuzungumza na washereheshaji wa sherehe (ma-MC), hasa harusi na viongozi wa nyumba za ibada ili waweze kutumia maeneo yao kuwakumbusha wadaiwa hao walipe madeni yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Abdul-Razaq Badru, alisema kuwa sasa ni wakati mwafaka kuhakikisha madeni yote yanalipwa kwa kutumia kila aina ya njia.

Aliwataka walionufaika na mikopo hiyo kuanza kujisalimisha wenyewe kulipa madeni yao kuepuka kusakwa majumbani na katika nyumba za ibada.

“Tumefanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa kuwashirikisha washereheshaji katika shughuli mbalimbali pamoja na nyumba za ibada ili waweze kuwakumbusha wadaiwa wa bodi kurejesha mikopo na ifikapo Januari Mosi, mwakani majina na sura za wadaiwa sugu tutazichapisha gazetini.

“Si hilo tu, pia tutapita nyumba kwa nyumba nchi nzima, hasa muda wa jua linapozama ili kuweza kuwafikia wadaiwa wote ambao walipata mikopo kupitia Bodi ya Mikopo. Mkopo si zawadi ni lazima ulipwe.

“Walipe ili na wengine waweze kunufaika na fursa ya mikopo. Na wale ambao watakaidi tutawafikisha mahakamani ambako watalipa gharama za uendeshaji wa kesi pamoja na deni wanalodaiwa,” alisema Badru.

Mkurugenzi huyo alisema hivi sasa wameanza utekelezaji wa marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ambapo kwa sasa wanufaika wa mkopo watalazimika kukatwa asilimia 15 badala ya asilimia nane ya awali.

Badru alisema sheria hiyo mpya imeipa meno bodi hiyo pia kuwawajibisha na kuwafikisha mahakamani waajiri endapo watashindwa kukata makato kwa waajiriwa wao ambao ni wanufaika wa mikopo au kuchelewesha kuwasilisha fedha za makato hayo.

“Kwa mabadiliko haya ya sheria, mwajiri sasa ana wajibu wa kuwasilisha majina, kukata na kuwasilisha makato stahiki kutoka katika mishahara ghafi ya waajiriwa wake walionufaika na mikopo ya elimu ya juu,” alisema Badru.

Alisema kwa waajiri ambao hawatawajibika, watalipa faini isiyopungua makato hayo au kifungo cha miezi 36.

Badru alisema pia wametoa siku 14 kuhakikisha kila mwajiri anapitia kumbukumbu zake na kuangalia kiasi walichokata na kuwasilisha katika bodi hiyo kabla timu iliyoundwa kufuatilia madeni hayo haijaanza kufanya kazi.

Alitoa wito kwa waajiri na waajiriwa kuhakikisha wanakusanya kumbukumbu muhimu ili kuepusha usumbufu endapo wataajiri wadaiwa sugu wa bodi hiyo na wakakwepa kutoa taarifa zao mapema.

Alisema kuhusu wanufaika ambao hawapo kwenye mfumo rasmi na mikopo yao imeiva, watalazimika kulipa Sh 100,000 au asilimia 10 ya kipato kinachotozwa kodi kwa mwezi.

“Sheria hii imepita mikononi mwa wadau ambao wamejaribu kupunguza ukali wa maisha, ambapo kwa wanufaika ambao hawako kwenye mfumo rasmi watalazimika kulipa deni lao baada ya miaka miwili badala ya mmoja wa sasa na kwa wale ambao wana ajira wataanza kulipa mara baada ya kuajiriwa,” alisema Badru.

Sambamba na hilo, bodi hiyo imesema hadi sasa  imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 140 kutoka kwa wanufaika wa mikopo iliyoiva. Awali deni lilikuwa ni Sh bilioni 300.

Mkurugenzi huyo alisema kiwango cha makusanyo ya mikopo ambayo awali yalikuwa ni Sh bilioni 2 kwa mwezi, hadi kufikia Novemba, mwaka huu yameongezeka na kufikia Sh bilioni 8 kwa mwezi.

Pia wadaiwa sugu waliojitokeza kulipa au kupunguza madeni yao wamefikia 42,700 kati ya 100,000 waliokuwa wanadaiwa awali.

“Katika kuhakikisha waajiri wanakusanya makato yetu, tumekutana na waajiri zaidi ya 10 na kuzungumza nao, ambao wengi wao walikuwa hawafahamu wajibu wao,” alisema Badru.

Kwa upande wa mwanasheria wa bodi hiyo, Luhano Lupogo, alisema mwajiri ana wajibu wa kupeleka makato ya mwajiriwa wake kwa bodi ndani ya siku 15, vinginevyo atalipa faini isiyopungua makato au kifungo cha miaka mitatu jela.

Alisema sheria hiyo ya mwaka 2004, namba 21 (2) imeanza kutumika Novemba 18, mwaka huu ambapo pia mwajiri ana wajibu wa kuwasilisha katika bodi orodha ya waajiriwa wake ambao ni wahitimu wa Stashahada au Shahada.

 

WANAFUNZI CHINA KUKOSA MIKOPO

Wakati huohuo, Mwandishi JOHANES RESPICHIUS anaripoti kuwa bodi hiyo imesema haitatoa mikopo kwa wanafunzi wote wa Tanzania waliofadhiliwa masomo katika nchi rafiki, ikiwamo China.

Hiyo ni kwa mujibu wa barua ya Desemba 20, mwaka huu iliyokuwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa imesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, kwenda ubalozi wa Tanzania nchini China.

Barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Kuchelewa kwa Fedha za Malipo kwa wanafunzi wanaosoma nchini China’, ilisema kuwa bodi hiyo haikupanga mikopo kwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma China kutokana na maelekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

“Kupitia barua ya wizara Kumbu. Na FB.54/283/01A/82 ya Septemba 14, mwaka huu, ilielekeza wanafunzi wote watakaopata ufadhili wa masomo (scholarship) kutoka katika nchi rafiki watakuwa wanajitegemea katika kununua tiketi za ndege kwenda masomoni.

“Pia barua hiyo ilielekeza kwamba wanafunzi wanaosoma katika nchi hizo hawatanufaika na mikopo ya nyongeza ya ada (topping up loan) kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” ilieleza barua hiyo.

Ilieleza kuwa kutokana na maelekezo hayo, bodi imeshindwa kupanga mikopo kwa wanafunzi hao waliopata ‘scholarship’ kwa mwaka wa masomo 2016/17 na wale waliokuwa wakiendelea na masomo China hadi itakapopata maelekezo zaidi.

MTANZANIA lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa HSELB, Badru ili kupata ufafanuzi zaidi wa suala hilo.

“Siwezi kusema ndiyo ni ya kwetu au hapana kwa sababu barua hiyo sijaiona, kwanza bodi haina utaratibu wa kuweka barua kwenye mitandao ya kijamii.

“Kama ina taarifa yoyote inataka kuitoa huwa inatumia utaratibu wa kawaida wa utoaji taarifa na kama kuna umuhimu kuweka kwenye mitandao ya kijamii ndipo huweka,” alisema Badru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles