Hellen Gerald (TUDARCo) -Dar es salaam
BAADA ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Biashara United, Amri Said amesema ubutu wa washambulaji wake ndiyo chanzo kikubwa cha matokeo hayo kutokana na kupoteza nafasi nyingi za kufunga mabao.
Biashara United inashika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi hiyo bila alama yoyote licha ya kushuka dimbani mara mbili, ikipokea vichapo vya 2-0 na 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na Mbao FC.
Said aliliambia MTANZANIA jana kuwa timu yake imekuwa ikicheza vizuri, lakini inaangushwa na makali dhaifu yanayoonyeshwa na washambulaji wake, akikiri kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa ya kupoteza pointi sita hadi sasa.
“Ni kweli nina changamoto kubwa ya washambuliaji kushindwa kufunga mabao, michezo yote hiyo tuliyopoteza siyo kwamba tulicheza vibaya, tulipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao kitu ambacho kimetugharimu.
“Bado ninaendelea kulifanyia kazi suala hilo kuhakikisha narudisha makali yao, tunajipanga kwa ajili ya kusaka pointi tatu za kwanza katika mchezo ujao dhidi ya Alliance, tutarekebisha makosa hayo ili tushinde,” alisema kocha huyo wa zamani wa Lipuli FC.