MOGADISHU, SOMALIA
VIKOSI vya Afrika vinavyolinda amani nchini hapa, AMISOM vimekanusha kuhusika katika kukamatwa kwa kiongozi wa zamani wa kundi la al Shabaab na kusababisha machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 11 na kujeruhiwa wengine kadhaa.
Taarifa hiyo imekuja kufuatia kuwapo kwataarifa zinazodai kuwa vikosi vya Ethiopia vilihusika katika harakati hizo kumkamata kiongozi huyo, Mukhtar Robow.
Pia taarifa hiyo imekuja muda mchache baada ya Spika wa Bunge la hapa, Mohamed Mursal Abdirahman, kutaka Robow aachiwe huru na huku akitoa rai uchaguzi waMkoa wa Kusini Magharibi ambako kiongozi huyo alikuwa mgombea usogezwe mbele.
Juzi Wizara ya Ulinzi wa Ndani ilisema kuwa imemkamata Robow ikimshutumu kuwarejesha wapiganaji wa Kiislamu na silaha katika mji wa Baidoa ambao ndio mji mkuu wa mkoa huo wa Kusini Magharibi.
Msemaji wa Robow alisema kuwa kiongozi huyo alipigwa na vikosi vya Ethiopia ambavyo ni sehemu ya kikosi hicho cha kulinda amani kabla ya kumkamata.
Mbalina msemaji huyo, viongozi na wakazi wa eneo hilo wanadai kuwa wanajeshi wa Ethiopia walisaidia kufanikisha kukamatwa kwa kiongozi huyo.
“Wanajeshiwa AMISOM hawakuhusika katika kumkamata Robow na wala kumsafirisha hadi Mogadishu,” ilieleza taarifa ya jeshi hilo na ikaongeza kwamba itaendelea kuheshimu uhuru wa watu na taifa la Somalia.