25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyetuhumiwa kwa upotevu wa Sh milioni 889 za chama cha ushirika ajiua

Nyemo Malecela – Kagera

ALIYEKUWA Meneja wa Chama cha Ushirika cha Ngara Farmers Cooperative, Humphrey Kachecheba (50), amekutwa amejiua katika nyumba ya wageni kwa kile kinachodaiwa alikuwa anakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na kufukuzwa kazi na kufunguliwa kesi mahakamani kwa upotevu wa fedha Sh milioni 889 mali ya chama hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, alisema mwili wa meneja huyo wa zamani wa chama hicho uligundulika Februari 3, mwaka huu saa tatu usiku akiwa chumba namba saba katika nyumba ya kulala wageni ya New Praise Lodge iliyopo Hamgembe, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Katika uchunguzi wa awali wa polisi, Kachecheba ambaye alikuwa mkazi wa Bunazi Kyaka, alichukua chumba katika nyumba hiyo ya wageni Januari 29, mwaka huu saa 4 asubuhi akitokea Wilaya ya Ngara alikokuwa akifanyia kazi na aliendelea kuishi hapo hadi alipogundulika amefariki dunia.

“Kwa muda wote inadaiwa alikuwa anashinda ndani ya chumba hicho amelala kila siku na kutoka saa 2 usiku na kurudi saa 4 usiku,” alisema Kamanda Malimi.

Alisema mwili wa Kachecheba uligunduliwa na mhudumu na nyumba hiyo ya wageni, Odetha Edmund wakati alipotaka kufanya usafi ndani ya chumba hicho, baada ya kugonga mlango bila kupata majibu kutoka kwa mteja wake huku mlango ukiwa umefungwa kwa ndani.

“Odetha alilazimika kusubiri hadi saa 10 jioni ambapo alirudia kumgongea, lakini bado Kachecheba hakufungua ndipo alitoa taarifa kwa meneja wake ambaye naye alitoa taarifa polisi ambao walifika na kuvunja mlango ambapo walimkuta tayari amefariki akiwa ametokwa na mapovu mdomoni,” alieleza Kamanda Malimi.

Alisema chanzo halisi bado kinachunguzwa, lakini hata hivyo kuna ushahidi mkubwa kuwa alijiua kwa sumu kutokana na msongo wa mawazo kufuatia kufukuzwa kazi na mwajiri wake jambo ambalo limethibitishwa na barua aliyokutwa nayo.

Kamanda Malimi alisema barua hiyo ya kufukuzwa kazi na mwajiri wake ambaye ni Chama cha Ushirika cha Ngara Farmers Cooperative ya Wilaya ya Ngara ilitolewa Desemba 12, mwaka jana kwa tuhuma za upotevu wa Sh milioni 889.

“Mbali na kufukuzwa kazi, lakini pia mwajiri wake huyo alimfungulia kesi mahakamani ambayo bado inaendelea.

“Katika uchunguzi wa awali katika chumba hicho alichokuwa amepanga Kachecheba, kulikutwa kifungashio cha madawa ya binadamu na masalia ya vimiminika vya kijani na vyeusi ndani ya chupa,” alisema Kamanda Malimi.

Aliongeza kuwa mwaka jana baada ya Kachecheba kutuhumiwa kuhusika na upotevu wa fedha hizo, alifanya jaribio la kutoroka, lakini alikamatiwa Bukoba na kurudishwa Ngara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles