28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

EU waachia Sh bilioni 132 walizokuwa wamezuia

Mwandishi wetu – Dar es Salaam

BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Manfred Fanti, amesema wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa umoja huo kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania ambapo Sh bilioni 132 zilizokuwa zimezuiwa zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka saba utakaoanza mwaka huu.

Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Ikulu, ilisema balozi huyo alisema hayo alipokutana Ikulu Dar es Salaam na Rais Dk. John Magufuli.

Fanti alisema mazungumzo yake na Rais Magufuli yamekuwa na manufaa makubwa ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na EU.

Alisema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania, ana matumaini kuwa EU itaendelea kufanya nayo kazi kwa ukaribu zaidi ili kufanya vizuri zaidi.

Rais Magufuli alimshukuru Fanti kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU.

Amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye masilahi kwa pande zote mbili.

CHINA NA CORONA

Aidha Rais Magufuli alikutana na Balozi wa China nchini, Wang Ke na kumkabidhi barua aliyomwandikia Rais Xi Jinping, akimpa pole kwa janga la homa ya virusi vya Corona lililolikumba Jiji la Wuhan nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Rais Magufuli alisema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.

 “China ni ndugu zetu, ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Balozi Ke alimshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki.

Alisema Serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo, imefanikiwa kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.

Alimhakikishia Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa virusi vya Corona, Watanzania 400 waliopo katika Jiji la Wuhan ambao wengi wao ni wanafunzi, hawajaambukizwa homa hiyo na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk. Stergomena Tax, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Fanti na Balozi wa China, nchini Ke, Ikulu Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo yake na Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Dk. Tax alisema alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya jumuiya hiyo, ikiwamo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara ambapo wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Dk. Tax alisema baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa SADC ni kuendeleza miundombinu, hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi wanachama, lakini ameipongeza Tanzania kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ikiwamo ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles