25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyemlipua Trump ni ofisa wa CIA

Washington, Marekani

SIKU chache baada ya mazungumzo ya simu ya Rais wa Marekani, Donald Trump yanayotajwa kuwa na nia ya kumsambaratisha mpinzani wake kisiasa, Joe Biden kunaswa, imebainika kuwa aliyevujisha mawasiliano hayo ya siri ni ofisa wa Shirika la Kijasusi la CIA

Trump anadaiwa kufanya mazungumzo hayo na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa nia ya kumtengenezea kashfa Biden anayepambana naye katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Ofisa huyo wa CIA aliyemlipua Trump hadi kusababisha Congress kuanzisha uchunguzi dhidi yake ambao unaweza kumwondoa madarakani bado hajatajwa jina lakini alipata kufanya kazi Ikulu.

Ofisa huyo amesema maofisa wa Ikulu ya Marekani (White House) walijaribu  kuzima mazungumzo ya hayo ya simu kati ya Trump na Rais wa Ukraine.

Chanzo cha habari kilicho karibu na majasusi kimeeleza kuwa Trump ametaka kujua ni nani aliyempa taarifa hizo ofisa huyo wa CIA aliyemlipua.

Kauli ya Ofisa huyo imekuja siku moja baada ya White House kutoa taarifa ya kina juu ya mazungumzo ya simu baina ya Trump na mwenzake wa Ukraine.

Taarifa ya White House imethibitisha kuwa, Julai 25, Trump alimuomba Rais Volodymyr Zelenski kumchunguza Biden anayesaka tiketi ya urais kupitia chama cha Democrats, ambaye mtoto wake alikuwa akifanya kazi na shirika la gesi la Ukraine.

Kwa mujibu wa mukhtasari, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mtoto wa, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

“Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo,” Trump ananukuliwa akisema kwenye mazungumzo hayo na kuongeza:

“Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

“Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo…ni jambo baya sana kwangu.” Anadaiwa kusikika Trump katika mazugumzo hayo

Zelensky naye anaripotiwa kujibu”Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

“Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana.”

Akimshukuru Trump, Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.

Hata hivyo Malalamiko hayo, yaliyotolewa Alhamisi, yanasema maandishi ya simu yaliyotolewa na Ikulu hayakuhifadhiwa katika mfumo wa kawaida wa kompyuta.

Badala yake yalihifadhiwa katika mfumo tofauti uliotumiwa na habari zilizoainishwa.

Trump ambaye anatoka chama cha Republican, anakataa kufanya jambo lolote baya na amepuuza mpango wa kutaka kumwondoa madarakani  

Licha ya kukubali kwamba alizuia mpango wa karibu Dola za Marekani milioni 400 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine kabla ya kuzungumza na Zelensky,  lakini anakataa kama uamuzi huo haukuwa shinikizo  kwa kiongozi huyo wa Ukraine kumchunguza Biden.

Mwanasheria wa Ofisa huyo wa CIA ameonya kuwa kumweka wazi mteja wake kunaweza kumuumiza.

Mashirika la kihabari ya The New York Times, Washington Post, na Reuters news yamemtaja aliyetoa taarifa hizo za siri kuwa ni ofisa wa CIA.

Wakati huo huo sauti iliyorekodiwa inasikika Trump akitaka kumjua mtu aliyevujisha taarifa hizo kwa mtu huyo.

” Ninataka kujua ni nani huyo mtu, ni mtu gani aliyempa mtu huyo taarifa. Kwa sababu huyo yuko karibu na majasusi,” alisikika Trump katika kikao chake binafsi na wafanyakazi wa Ikulu katika alichofanyia katika moja ya ofisi za  UN.  Sauti hiyo iliyorekodiwa inapatikana Los Angeles Times.

Akielezea kazi ilivyokuwa ikifanywa na majasusi wa Marekani zamani Trump pia amesikika akisema: ” Unajua tulichokuwa tunafanya siku za nyuma tulikuwa smart? sawa? upelelezi na uhaini, tulikuwa tukishughulikia kidogo tofauti na tunavyofanya sasa…”

Kauli hizo zimelaaniwa vikali na wenyeviti wa kamati tatu za Democrat katika Baraza la wawakilishi.

Katika taarifa yao ya pamoja walisema kauli hizo  ni “vitisho dhidi ya shahidi” na jaribio la kuzuia uchunguzi wa mashtaka yanayomkabili yeye Trump.

Mjumbe mmoja wa Democrat alisema anataka mtoa taarifa huyo za siri azungumze na kamati ya usalama mapema.

“Nina wasiwasi na baadhi ya kauli za rais anazozitoa dhidi ya mtu huyo aliyetoa taarifa za siri, na huenda akalipiza kisasi dhidi ya huyo mtu,” alisema Raja Kirshnamoorthi.

Mtoa taarifa huyo anamtuhumu Trump kutumia madaraka yake kuharibu uchaguzi wa Marekani wa 2020 kwa kutumia nchi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles