LIVERPOOL, ENGLAND
MLINDA mlango namba moja wa timu ya Liverpool, Alisson Becker, anatarajia kuwa kwenye kikosi cha timu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United baada ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili.
Kipa huyo raia wa nchini Brazil, alipata majeruhi kwenye mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa michuano ya Ligi Kuu England dhidi ya Norwich kwenye uwanja wa Old Trafford. Aliumia nyama za paja dakika ya 37.
Kocha wa timu ya Liverpool, Jurgen Klopp, ameweka wazi kwamba, alikuwa na nafasi ya kumchezesha kipa huyo kwenye mchezo dhidi ya Leicester City, ila alihofia hali yake, hivyo aliamua kumuacha afanye mazoezi kwa ajili ya mchezo wa mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Manchester United.
Kipa huyo alijiunga na Liverpool kwa kitita cha pauni milioni 64.6, wakati wa uhamisho wa kiangazi 2018 akitokea klabu ya AS Roma. Tangu ajiunge na timu hiyo amekuwa na mchango mkubwa wa mafanikio ikiwa pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, Liverpool haijapoteza mchezo kwenye michuano ya Ligi Kuu England tangu kuanza kwa msimu huu japokuwa kipa huyo alikuwa nje ya uwanja huku nafasi yake ikichukuliwa na Adrian Castillo, raia wa nchini Hispania.
Kwenye msimamo wa Ligi, Liverpool wanaongoza wakiwa na jumla ya pointi 24 baada ya kucheza michezo nane, huku mabingwa watetezi Manchester City wakishika nafasi ya pili baada ya kuvuna pointi 16.
Mchezo huo ambao utapigwa Jumapili wiki hii, Manchester United watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani Old Trafford, ambapo United wanatakiwa kushinda ili kulinda kibarua cha kocha wao Ole Gunnar Solskjaer. Kwa sasa Manchester United wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare mitatu na kupoteza mitatu.