ALGIERS, Algeria
SERIKALI ya Algeria imesitisha usafirishaji wa gesi kupitia kwa majirani zao, Morocco, na hiyo yote imetokana na kuyumba kwa uhusiano kati ya mataifa mawili hayo.
Algeria imekuwa ikiitumia Morocco kusafirisha mabomba ya gesi kuelekea Hispania. Si tu Morocco imekuwa ikinufaika kwa kulipwa, pia hutumia gesi hiyo kuzalisha asilimia 10 ya umeme wake.
Hatua ya kuondoa ushirikiano huo inakuja baada ya mkataba wa pande mbili kufikia ukomo jana, hivyo mamlaka za Algeria kutoona umuhimu wa kuongeza mwingine.
“Kutokana na vitendo vya uadui vya Morocco dhidi ya Algeria, Rais ameagiza kampuni ya mafuta ya Sonatrach kusitisha uhusiano wa kibiashara na kampuni ya umeme ya ONEE,” inasomeka taarifa ya Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune.