Na MOHAMED HAMAD-KITETO
BENDERA Maguluko (55), mkazi wa Kiteto, mkoani Manyara, amesema anatarajia kwenda Ikulu, Dar es Salaam kumpelekea zawadi ya bata dume Rais Dk. John Magufuli, kutokana na utawala wake mzuri ambao umemfurahisha.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Maguluko alisema nia yake hiyo ni kuunga mkono jitihada za Rais za kupambana na mafisadi nchini.
“Kuna kila sababu ya Watanzania kutambua mchango wa Rais Dk Magufuli, binafsi natoa shukrani za dhati kwa Mungu, kwani kazi anayofanya ni kubwa na inapaswa kuungwa mkoani na watu wenye nia njema,” alisema.
Aidha, Maguluko alizitaja baadhi ya kazi zilizofanywa na Dk. Magufuli kuwa ni pamoja na kukabiliana na watumishi hewa, wanafunzi hewa, Serikali kuhamia Dodoma, ununuzi wa ndege sita za Serikali, kufuta baadhi ya sherehe zilizowagharimu wananchi, pamoja na maboresho ya elimu, afya, maji na miundombinu mingine.
Mwananchi mwingine, Maulidi Kijongo (58), alisema viongozi wengine wa Serikali wa ngazi mbalimbali wasiendelee kumshangaa Rais Mgufuli kwa kazi anayofanya, badala yake kila mtu awajibike katika nafasi yake, ili wananchi waweze kunufaika na utawala huo.
“Kila kona ya nchi wananchi wengi wamekuwa wakimsubiri Rais Magufuli kutatua matatizo yao, kana kwamba hakuna viongozi wengine katika maeneo hayo,” alisema.