29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali zaua watu 860 kwa miezi mitatu

mtanzaniadaily afcon.inddKOKU DAVID NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES ALAAM
JESHI la Polisi nchini, limesema Watanzania 866 wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu, kutokana na ajali za barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ajali 2,116 zimetokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema katika ajali hizo, watu 866 wamepoteza maisha na wengine 2,363 kujeruhiwa, ambao baadhi yao wamepata ulemavu.
Hata hivyo nje na kipindi hicho, ajali nyingine zilizotokea kuanzia Machi 11 hadi April 12, mwaka huu zimesababisha vifo vya watu wengine 103 na hivyo kufanya idadi ya watu walipoteza maisha katika kipindi cha miezi mine kuwa 969.
Akizungumzia sababu za ajali hizo, Kamanda Mpinga alisema ni mwendo kasi usiozingatia alama za barabarani na kufutika kwa baadhi ya michoro barabarani.
Alisema sababu nyingine, ni baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto kuhamasisha mwendo kasi kwa madereva wao, abiria kushabikia na baadhi ya wadau wa usalama barabarani kutowajibika ipasavyo.
Kamanda Mpinga, alisema uzembe wa madereva, ubovu wa barabara na uoni hafifu kwa baadhi ya madereva ni miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi kutokea.
Alisema kuwapo kwa tatizo la utelezi, ulevu na uchovu, unaosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha nako kumeongeza idadi ya ajali.
“Utumiaji wa dawa za kulevya ni sababu nyingine ambayo inasababisha ajali nyingi,” alisema.
Huku akionekana kusikitishwa na matukio hayo, Kamanda Mpinga alisema tatizo jingine ni ubabe wa madereva wanaoendesha magari makubwa ya mizigo kutothamini magari ndogo, waenda kwa miguu, bajaj pamoja na pikipiki wawapo barabarani.
HATUA KALI
Kuhusu hatua, Kamanda Mpinga, alisema madereva wote waliosababisha ajali za hivi karibuni watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni zao.
Alisema ajali nyingine zitakazotokea baada ya hizo, wamiliki wa vyombo husika watafungiwa kampuni zao.
Alitoa wito kwa watumiaji wa barabara kuchukua hadhari, madereva kuwa makini msimu huu wa mvua.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wamiliki wa mabasi yanayokwenda safari za mbali kuajiri madereva wawili watakaosafiri ili kumpunguzia dereva uchovu.
Aliomba Bunge
Ili kukomesha au kupunguza wimbi la ajali hizo, Kamanda Mpinga ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubadilisha sheria zilizopo za usalama barabarani ambazo zinatoa adhabu ndogo kwa watu wanaosababisha ajali.
Alisema uchunguzi uliofanywa na kikosi hicho, umebaini wamiliki wa mabasi wamekuwa wakihamasisha madereva wao kwenda mwendo kasi kwa kujali maslahi yao kibiashara zaidi.
Miongoni mwa ajali zilizogusa mioyo ya watu ni ile iliyotokea Machi 11, mwaka huu katika Kijiji cha Changarawe Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ambapo watu 50 walipoteza maisha, huku 20 wakijeruhiwa kutokana na basi la Majinja kugongana na lori.
Katika ajali nyingine iliyotokea maeneo ya Mikumi Mbugani mkoani Morogoro Machi 17, mwaka huu na kuhusisha basi la Fm Safari na lori aina ya Scania, watu wawi walipoteza maisha na nane kujeruhiwa.
Ajali nyingine ilitokea Machi 19, mwaka huu eneo hilo hilo la Mikumi na kuhusisha basi dogo aina ya Tata linalojulikana kwa jina la Msanga Line lililogongana na basi la Luvinzo na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi 17.
Ajali nyingine ni ile iliyotokea Aprili 3, mwaka huu iliyokuwa imebeba mashabiki wa timu ya soka ya Simba ambao walikuwa wakielekea mkoani Shinyanga, ambapo iliua watu saba na kujeruhi 22.
Mbali na ajali hizo, ajali nyingine iliyotokea mkoani Tanga eneo la Mkata ilihusisha basi la Ratco, Ngorika na gari dogo aina ya Paso ambapo watu 10 walipoteza maisha pamoja na kujeruhi wa 12.
Pia Aprili 12, mwaka huu mkoani Morogoro kulitokea ajali katika milima ya Hiyovi ambapo basi la Nganga Express lililogongana na Fuso na baadaye kuwaka moto na kusababisha watu 19 kupoteza maisha, huku wengine 10 wakijeruhiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles