27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Taasisi za dini kufutwa

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imetishia kuzifutia usajili taasisi mbalimbali za kidini, endapo zitabainika kukiuka sheria ya vyama vya kijamii kwa kutoa matamko na kushawishi waumini wao kutekeleza matakwa ya kisiasa.
Kauli ya Serikali, imekuja siku chache baada ya viongozi wa Jukwa la Kikristo Tanzania (PCT) kutoa tamkoa la kuwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana Katiba inayopendekezwa, wakisema imeandaliwa kwa njia ya ubabe.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema kitendo kinachofanywa na taasisi hizo ni kinyume cha sheria ya vyama vya kijamii Sura ya 337 na kanuni zake inayosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Chikawe alisema Serikali haifanyi mzaha katika suala hilo na kueleza kwamba kuanzia Aprili 20, mwaka huu taasisi zitakazoshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za mwaka pamoja na kulipa ada zao zitachukuliwa hatua.
Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na matukio ambapo baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakitoa matamko yenye sura ya kisiasa kinyume cha sheria hiyo.
“Ni kweli viongozi wa taasisi za dini, wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kuwashawishi waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa.
“Waumini wa dini mbalimbali wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao, wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao wenyewe bila ya kushawishiwa na mtu yeyote kama sheria za nchi zinavyotaka.
“Mfano mwingine ni pale viongozi wa dini wanapochangisha fedha na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, hii si kazi ya taasisi za dini na ni kinyume cha sheria.
“Kwa mfano viongozi wa taasisi hizi, wanapokutana na kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba inayopendekezwa au uchaguzi mkuu ujao, matamshi kama hayo yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo,” alisisitiza Chikawe.
Aliongeza. “Tutachukua hatua ya kuvifutia usajili vyama vyote vya kijamii vilivyosajiliwa chini ya sheria, Sura 337… ambavyo vitakiuka katiba za kuanzishwa kwake na ambavyo havifuati matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada zao kuanzia Aprili 20, mwaka huu,” alisema.
Bakwata, TEC, waivutia pumzi
Hata hivyo baadhi ya viongozi taasisi mbalimbali za kidini wameonesha kukerwa na tamko hilo, huku wengine wakipinga mtazamo huo.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Tarcisius Ngalalekutwa alipoulizwa kuhusu kusudio hilo la Serikali, alisema bado tamko hilo halijawafikia wao kama viongozi wa dini.
“Sijapata taarifa yoyote kuhusu tamko hilo, lakini ngoja tusubiri ilitoe halafu tuone ili tujue kilichoendelea,” alisema Ngalalekumtwa ambaye pia ni Askofu wa Kanisa Katoliki mkoani Iringa.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Bin Simba alisema taarifa hizo bado hazijalifikia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
“Ndiyo kwanza unaniambia ndiyo maana nashindwa kusema lolote ni vema nione tamko lenyewe la Serikali halafu nijue cha kuzungumza, lakini kwa sasa siwezi,”alisema Simba.
Hata hivyo, Msemaji wa Baraza Kuu, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba alipinga hoja ya kuzuia masuala ya siasa katika nyumba za ibada.
Alisema si sawa kuzuia waumini wasihubiri masuala ya kisiasa ndani ya nyumba za ibada, kwa kuwa taasisi hizo zinafanya kazi za kila siku na wananchi.
“Huwezi kuwaambia viongozi wa dini wasizungumze masuala la siasa, wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu wako karibu na waumini ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa,”alisema Sheikh Katimba.
Alishauri serikali kuliangalia kwa undani suala hilo kabla ya kulitolea uamuzi ili lisije kuleta mtafaruku katika jamii na taasisi za dini zenyewe.
TAMKO LA PCT
Machi 12, mwaka huu, Jukwa la Kikristo Tanzania (PCT) linaloundwa na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) walitoa tamkoa la kutounga mkono Katiba inayopendekezwa na kudai kuwa imeandaliwa katika mazingira yasiyokuwa ya kiuadilifu.
Mbali na hilo, pia walisema Katiba hiyo ikipitishwa italeta mgawanyiko mkubwa katika taifa kwa sababu mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe.
Waraka wa baraza hilo, kwa vyombo vya habari ulisainiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa kwa niaba ya (CCT), Rais wa Baraza la Maaskofu Katholiki Tanzania Tracius Ngalalekumtwa (TEC), pamoja na D. Aweti kwa niaba ya wapentekoste (CPCT).
Taarifa hiyo ilisema kutokana na hali hiyo, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba inayopendekezwa hivyo kuwataka waumini wao kupiga kura ya hapana wakati wa kura ya maoni iliyotarajiwa kufanyika April 20 mwaka huu kabla ya kuahirishwa kutokana na kuchelewa kwa uandikishaji wa Datfari la Kudumu la Wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki (BVR).
Waraka huo, ulisema Katiba inayopendekezwa haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala mbalimbali yanayohusu muundo wa Serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais, uwiano wa mihimili ya dola.
“Kutokana na hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana kwa Katiba inayopendekezwa”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles