Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
DUNIANI kuna watu wa jinsia mbili yaani ya kike na ya kiume, ambazo huzaliwa nazo.
Hali hiyo inaelezwa kibaiolojia si jambo la kawaida na hutambulika kuwa ni tatizo la jinsia tata ambalo kitaalamu huitwa ‘Ambiguous Genitalia’.
Ni neno linalotumika kueleza viungo vya siri vya mtoto aliyezaliwa ambavyo ni vigumu kujua ni wa jinsia ya kike au ya kiume.
Mtoto wa kike mwenye tatizo hilo huzaliwa na kiungo kinachofanana na uume, mfuko wa korodani na kwamba tundu la njia ya uzazi huwa halionekani kabisa.
Aidha, mtoto wa kiume mwenye tatizo hilo, huzaliwa na tatizo la kutokufunguka kwa njia ya mkojo mwishoni mwa uume, uume kuwa mfupi, kutokuwepo kwa korodani ndani ya vifuko vyake au kuwa na uwazi katikati ya korodani.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaitun Bokhari anasema tatizo hilo huwaathiri zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume.
Anasema kitaaluma punde tu baada ya mama kujifungua daktari au mkunga huwajibika kumnyanyua mtoto na kumuonesha ili atambue jinsia ya mtoto wake.
“Moja kwa moja mama hupeleka macho yake eneo la sehemu ya siri ya mwanawe na anapoona anataja jinsia aliyoiona kama ni wa kike au wa kiume,” anasema.
Anasema katika hatua hiyo ni vigumu mno mama kubaini kasoro ikiwa mtoto wake amezaliwa na tatizo la jinsia tata.
“Nimesema awali kwamba tatizo hili linawalabili zaidi watoto wa kike kuliko wa kiume, kwa sababu mama anapomuangalia mtoto pale anapooneshwa akiona uume umechomoza moja kwa moja anasema ni wa kiume na asipouona anasema ni wa kike.
“Si rahisi kugundua kwa sababu unaweza kukuta mtoto wa kike anazaliwa akiwa na kinena kikubwa kuliko kawaida kiasi kwamba mtu anaweza kukifananisha na uume wa mtoto mchanga.
“Mtoto wa aina hiyo, anakuwa na mashavu ya uke kama kawaida na yale matundu muhimu kwenye uke au wakati mwingine unakuta yale mashavu yameungana.
“Lakini ukimwangalia kule chini unakuta ana njia ya haja ndogo kama kawaida, ni maumbile yenye utata hivyo kutokana na hali hiyo ndiyo maana ni vigumu mama kutambua kasoro pale anapooneshwa mtoto wake punde tu baada ya kujifungua,” anasema.
Wakati wa ukuaji
Dk. Bokhari anasema kwa kuwa wazazi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu tatizo hilo, huendelea kulea watoto wao wakidhani ni hali ya kawaida kumbe la.
“Hushindwa kutambua mapema kwamba ni tatizo linalohitaji kutafutiwa ufumbuzi mapema, hudhani ni hali ya kawaida na wengine hudhani watoto wao wapo katika hali hiyo kutokana na unene, kumbe ni tatizo,” anasema.
Anaongeza: “Kwa hiyo, unakuta mtoto analelewa kama vile wa kiume kumbe ni wa kike au analelewa kama wa kike kumbe ni wa kiume.
Chanzo chake
Tatizo hilo linaweza kusababishwa na ongezeko la homoni za kiume kwa mtoto wa kike au za kike kwa mtoto wa kiume wakati akiwa tumboni mwa mama yake.
Hali hiyo husababisha muonekano wa viungo vya nje na tabia visiendane na viungo vya uzazi vya ndani na aina ya jinsia kwenye vinasaba.
“Kwa kawaida, jinsia ya mtoto hutegemea ile mbegu ya baba imebeba vinasaba vya kike au vya kiume,” anasema Profesa Sten Drop.
Anasema jinsia ya mtu hutokea mara tu baada ya mimba kutungwa hata hivyo, viungo vya ndani na vya nje vya uzazi hutegemea homoni ambazo zimebebwa kwenye vinasaba.
Profesa Drop anasema ikiwa itatokea hitilafu yoyote katika vinasaba, husababisha homoni hizo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
“Hali hiyo husababisha kutotengenezwa au kutengenezwa jinsia zote mbili kwa mtoto aliyepo tumboni mwa mama,” anasema.
Visababishi
Dk. Bokhari anasema hadi sasa bado haijulikani nini hasa husababisha kutokea kwa hitilafu katika vinasaba na hivyo mtoto kuzaliwa na tatizo hilo.
“Lakini kuna visababishi ambavyo huweza kuchangia mtoto kuzaliwa na tatizo hili, hasa magonjwa ambayo mama huugua kipindi cha ujauzito na anapokosa virutubisho muhimu kipindi cha ujauzito.
“Kiujumla afya ya mama ni jambo la msingi mno ili kumuepusha mtoto kuzaliwa na tatizo hili, mama akiwa na afya duni huchangia kwa kiwango kikubwa uwezekano wa mtoto kuzaliwa na tatizo tata,” anabainisha.
Hali ilivyo MNH
Dk. Bokhari anasema kila mwezi hupokea watu watano hadi sita wanaokabiliwa na tatizo hilo katika kliniki yake.
“Muhimbili ni hospitali kubwa ya rufaa hivyo wagonjwa hao hutoka katika mikoa mbalimbali nchi nzima lakini changamoto ni kwamba huja wakiwa wamechelewa mno,” anasema.
“Tumeshapokea watoto wenye umri wa miaka mitatu, saba, nane na hivi karibuni tumepokea kijana mwenye miaka 29 ambaye amelelewa miaka yote hiyo kama mtoto wa kiume na tayari ana mpenzi wake na wanatarajia kufunga ndoa.
“Lakini mpaka amechukua hatua ya kuja hospitalini ni baada ya kuona anapatwa na hali tofauti na wavulana wengine, alishangaa kuona anapata hedhi hali ambayo kwa kawaida huwapata wanawake,” anasema.
Anasema walimfanyia uchunguzi kwa vipimo vya kibingwa ambavyo vilionesha ndani ya mwili wake kuna mfumo wa uzazi wa mwanamke na hana kabisa mfumo wa uzazi wa mwanamume.
“Kijana huyo ana uterasi (tumbo la uzazi), mirija yote miwili na vifuko vya mayai anavyo na tuliona kuna yai lilikuwa limeshapevuka tayari kupata hedhi,” anasema.
Athari zinazowakabili
Profesa Drop anasema watu waliozaliwa na tatizo hilo wanapokuja kugundulika ukubwani wengi hupatwa na matatizo ya kisaikolojia.
“Hukosa raha, wengi hutafakari namna ambavyo jamii itawanyanyapaa pindi itakapojua kuhusu tatizo lao, huwa na mawazo mengi mno, huhitaji ushauri nasaha kila wakati,” anasema.
Anasema hata wazazi waliopata mtoto mwenye tatizo la jinsia mbili huwa katika wakati mgumu.
“Kwa sababu wanakuwa wanajua mtoto wao labda ni wa kiume lakini vipimo vinaonesha ni wa kike, au wa kike lakini vipimo vinaonesha ni wa kiume.
“Hivyo hujiuliza maswali mengi hasa namna gani watamtuza mtoto wao kulingana na majibu ya vipimo huku jamii inayomzunguka ikifahamu kinyume chake,” anasema.
Anasema hata hivyo ni muhimu mno kwa wazazi kuwahi kumpeleka mtoto hospitalini kwa uchunguzi pindi tu wanapobaini kasoro.
“Katika nchi zilizoendelea tatizo hili hugundulika mapema na watoto wa aina hii hupewa matibabu mapema lakini naona hali ni tofauti katika nchi zinazoendelea,” anasema.
Dk. Bokhari anasema kutokana na uelewa mdogo juu ya tatizo hilo ni kweli watoto wengi hufikishwa hospitalini wakati umri ukiwa umekwenda.
“Ni changamoto ambayo tunaiona tofauti na wenzetu wa nchi zilizoendelea, wao wanawahi kugundua na wanatibiwa mapema,” anasema.
Kutokukubali matokeo
Anasema zipo jamii zingine ambazo hukataa kukubali matokeo ya vipimo vya kitaalamu kuhusu watoto wao.
“Kwa mfano; yupo mama mmoja, mtoto wake alichunguzwa hospitalini tangu siku alipozaliwa na madaktari walimueleza ana tatizo hili.
“Kadiri alivyokua yule mtoto alionekana kuwa na mwonekano wa mtoto wa kiume lakini jinsia ya kike, yule mama alikuwa akimlea kama mtoto wa kike.
“Lakini kipindi fulani ikabidi aende kijijini kuwasalimia wazee alipofika huko wale wazee walihoji kwanini anamlea mtoto kama wa kike wakati ni wa kiume.
“Wakamshinikiza amlee kulingana na malezi ya mtoto wa kiume na si wa kike, ikabidi afanye hivyo hadi aliporejea mjini na akaja hapa Muhimbili.
“Tukamchunguza tena mtoto vipimo vikaonesha ni wa kike ila mwonekano wake ni wa kiume, kwa hali ya namna hiyo moja kwa moja wazazi huathirika kisaikolojia.
“Yupo pia mama mwingine ambaye nimempa ushauri nasaha na kumfanya kuwa rafiki yangu ili niwe naye karibu zaidi, nikimshauri asijisikie vibaya kuwa na mtoto wa aina hiyo,” anasema.
Je, tiba ipo?
Profesa Drop anasema tatizo hilo linatibika kwa njia ya upasuaji na kwamba matibabu hayo huhusisha jopo la madaktari pamoja na wataalamu wa kisaikolojia.
“Lakini hutegemea hatua za tatizo ila ni muhimu wazazi kupatiwa ushauri wa kisaikolojia ili waweze kukabiliana na hali ya wasiwasi wanaoweza kuwa nao na kuwasihi kuwa wavumilivu kipindi cha kusubiri majibu ya vipimo,” anasema.
Anaongeza: “Madhara makubwa yanawapata hasa pale ambapo inabidi kubadili utambulisho wa jinsia ili kuendana na muonekano wao.
Dk. Bokhari anasema sheria inawapa ruhusa madaktari nchini kufanya upasuaji dhidi ya tatizo hilo.
“Hairuhusiwi kubadili jinsia kama vipimo vya uchunguzi havijaonesha muhusika ana tatizo, lakini hata kama mtu ana tatizo inabidi familia iliridhie.
“Na ikiwa ni mtu mzima japo tutamshauri lakini anaweza mwenyewe kuamua anataka kufanyiwa au la,” anabainisha.
Anasema hata hivyo wengi hushindwa kuamua kwa kuhofia unyanyapaa watakaofanyiwa kwenye jamii pale itakapogundulika kuwa walizaliwa na jinsia tata.
Kuhama mazingira
Anasema wakati mwingine hasa baada ya upasuaji hushauri wahusika kuhama au kuhamishiwa kwenda kuishi katika mazingira mengine tofauti na aliyokulia.
“Hii ni sehemu ya matibabu, kwa mfano kuna watoto wawili ambao tuliwagundua kuwa na jinsia tata, tukawatibu sasa ili kuwaepusha na ule unyanyapaa kutoka kwa jamii na wanafunzi wenzao tuliwashauri wazazi wao wawahamishe katika mazingira mengine. Wakahamishwa shule na hata makazi walihama,” anabainisha.
Anatoa rai kwa wataalamu wenzake wa afya hasa wauguzi, wakunga na madaktari kuwakagua kwa makini watoto mara baada ya kuzaliwa.
“Kiutaratibu baada ya mama kuoneshwa, wanatakiwa kumkagua mtoto kuanzia utosi hadi unyayo wake kujiridhisha amezaliwa salama au la, na wanapoona kasoro wampe mama rufaa ili akasaidiwe na wataalamu waliobobea zaidi,” anasema.
Anasema ni rahisi pia kwa mama kumkagua mtoto wake kwa kulinganisha maumbile yake ya kwake ikiwa ni wa kike au ya baba yake ikiwa ni wa kiume.
“Hata kama yatatofautiana ukubwa lakini ikiwa kuna kasoro atabaini tu, ni vema akibaini amuwahishe hospitalini,” anatoa rai.
Muhimu
Tatizo hilo huweza kurithiwa kwenye familia kwa sababu hutokana na hitilafu kwenye vinasaba.
Ni vizuri kujua kama kwenye familia kuna historia ya tatizo la jinsia tata au la.
Jambo jingine muhimu ni kujua iwapo mzazi mmojawapo ana tatizo la kimaumbile kwenye viungo vya uzazi.
Ni muhimu kujua iwapo mmojawapo ana historia ya kuchelewa kubalehe au kutopata hedhi mara kwa mara na mambo mengineyo.