23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI YA KUEPUKA MAUDHI YANAYOSABABISHWA NA DAWA

MATIBABU ya magonjwa mbalimbali yanahusisha matumizi ya dawa kama nyenzo muhimu katika kufikia lengo la tiba stahiki.

Katika kutumia dawa, kuna nyakati ambazo kunatokea maudhi ambayo yanakuwa kama kikwazo kwa mtumiaji wa dawa husika kwa kutegemeana na tatizo lake la kiafya. Mifano ya maudhi hayo ni kama vile ngozi kuwasha, kuhisi kutapika au kichefuchefu, kuvimbiwa (Constipation), kuhisi kama kuna vitu vinakwangua tumboni, kuvimba mwili na maudhi mengine tofauti.

Lengo la kutoa matibabu siku zote ni kwa dhumuni la kumsaidia mgonjwa. Utoaji wa matibabu kimsingi unafuata taratibu za kiafya ambazo zinazingatia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kulinganisha faida endapo mgonjwa atatumia dawa husika, hasara zinazoweza kujitokeza endapo mgonjwa hatotumia dawa husika, pia maudhi yanayoweza kujitokeza endapo mgonjwa atatumia dawa. Mambo yote haya kwa pamoja huzingatiwa katika kufanikisha matibabu ya mgonjwa na kumwezesha kuirejesha afya katika hali ya uimara zaidi.

Pamoja na kuzingatiwa mambo hayo katika matibabu, jambo la kukumbuka ni kwamba maudhi haya ya dawa hayatokei kwa kila mtu. Watu tofauti tofauti wanaweza kutumia dawa ya aina moja lakini, mtu mmoja akapatwa na maudhi hayo na mwenzake akabaki bila usumbufu wowote.

Ili kuweza kuepukana na maudhi haya na hatimaye ukatumia dawa kwa urahisi na ukamaliza dozi kwa ukamilifu wake, ni vyema kuzingatia mambo yafutayo:

Awali ya yote, sehemu kubwa ya mgonjwa kuweza kupata matibabu sahihi kwa maana ya dawa ni zoezi linalohitaji taarifa sahihi za mgonjwa zipatikane ambazo zinaelezea kwa kina kuhusu chanzo cha tatizo/ugonjwa na hali nzima ya ugonjwa hadi hapo ambapo amefikia hatua ya kuonana na mtaalamu wa afya/daktari. Pasipokuwapo na taarifa za kujitosheleza kutoka kwa mgonjwa kutapelekea kuathiri aina ya matibabu na dawa ambazo zitatolewa kwa mgonjwa. Hivyo, ni jukumu lako kama mgonjwa/mteja kutoa taarifa sahihi za tatizo lako ili uweze kupewa dawa sahihi na kuepukana na maudhi yasiyo ya lazima.

Kuna maudhi ya dawa ambayo husababishwa na upungufu wa mgonjwa katika kuitumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya dawa yanavyotakikana, sababu inaweza kuwa ni mgojwa kutopewa maelekezo sahihi au pengine kujisahau au kutozingatia maelekezo yanayotolewa.

Mfano wa maudhi ambayo yanaweza kujitokeza kwa kutotumia dawa kwa ufasaha ni kama vile kuhisi tumbo kujaa au kuvimbiwa, tumbo kukwangua.

Kwa aina hii ya maudhi, hutokea pindi mgonjwa anapokosea kutumia dawa kwa usahihi mfano dawa jamii ya vidonge vya kuongeza damu pamoja na dawa za maumizu.

Ili kuepukana na maudhi ya aina hiyo inashauriwa kutumia dawa za jamii hiyo (dawa za maumivu) nyakati ambazo tayari mgonjwa ameshakula chakula (tumboni kuwe na chakula). Pia kwa maudhi ya kuvimbiwa na kuhisi kichefuchefu baada ya kutumia dawa za kuongeza damu, inashauriwa kutumia dawa hizo sambamba na vyakula au vinywaji ambavyo husaidia dawa hizo kuyeyuka na kuingia katika mfumo wa damu kwa urahisi. Mfano wa vyakula na vinywaji hivyo ni kama vile nyama, vyakula vyenye asili ya uchachu au juisi za matunda.

Pia kuna maudhi ambayo yanatokea kwa mgonjwa ambayo hutokana na asili ya dawa yenyewe. Mfano, unaweza kuitumia dawa vizuri kwa maelekezo sahihi lakini bado maudhi kama vile ngozi kuwasha na kuhisi usingizi bado ukapata maudhi hayo.

Kwa aina hii ya maudhi hatua au tahadhari ambazo unaweza kuzichukua ili kuepukana na maudhi kama haya ni kama vile kutumia dawa nyakati za usiku muda wa kwenda kulala, hii ni kwa dawa ambazo zinakuletea usingizi pindi uzitumiapo. Mfano, dawa aina ya cetrizine ambayo imekuwa ikitibu tatizo la mafua na aleji. Kuna nyakati kwa baadhi ya watumiaji hupatwa na usingizi pindi watumiapo dawa hii. Angalizo la kubadili ratiba ya kutumia dawa ni kwa dawa ambazo hutumika mara moja kila baada ya saa 24 (mara moja kwa siku) pia ni vyema ukapata ushauri wa kitaalamu kabla ya kubadili ratiba ya utumiaji wa dawa yako. Aidha, kuna dawa ambazo zinaweza kutumika ili kupunguza maudhi ya dawa nyingine, mfano kuna dawa ambazo zinaweza kutumika kuondoa maudhi kama ya ngozi kuwasha, mwili kuvimba. Kwa dawa zenye kuleta maudhi ya aina hiyo njia ya kuepukana nayo ambayo inaweza kutumika ni kutumia dawa za aleji mfano chrolpheniramine au cetrizine.

Siku zote dawa hutolewa kwa mgonjwa ili ziweze kumsaidia na si kuwa kikwazo.

Kwa taarifa zaidi unaweza kutembelea: www.tanzlife.co.tz

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles