30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHANJO YA VIRUSI VYA UKWIMI  IKO NJIANI

JOSEPH HIZA NA MTANDAO


WANASAYANSI nchini Marekani wanakaribia kupata chanjo ya kuzuia maambukizo ya Virus Vya Ukimwi (VVU), utafiti mpya umekadiria.

Chanjo hiyo ya sindano moja ililinda nyani dhidi ya virusi kwa wiki 18, ikikadiria kuwa dozi ya sindano moja inaweza kutoa kinga ya miezi kadhaa kwa binadamu, utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Rockefeller, New York umebainisha.

Watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa kama vile wale wenye wenzi waishio na VVU, wanaweza kukingwa dhidi ya maambukizo na dawa hiyo inayoitwa PrEP kabla ya tendo la ndoa. Hata hivyo, hakuna chanjo iishiyo kwa kipindi kirefu kwa ufanisi.

Kutengeneza chanjo aina hiyo ni ngumu kutokana na VVU kuwa na tabia ya kujificha kutoka mifumo ya kinga ya watu, hata hivyo, protin fulani katika dozi husababisha chembe za kinga kutambua ‘bahasha’ inayozingira virusi, utafiti umeongeza.

Kwa mujibu wa watafiti, matokeo yao waliyochapisha katika Jarida la Nature Medicine, yameashiria mwelekeo mzuri wa kupatikana chanjo ya kuzuia maambukizo, ambayo inaweza kutolewa kidogo kidogo mara moja. Hata hivyo, haikuweza kujulikana lini chanjo hiyo itaanza kupatikana.

Dawa hii ni mseto wa dozi mbili zinazounda ARV; tenofovir na FTC.

Hufanya kazi pamoja kuingilia kimeng’enya ambacho VVU hutumia kuambukiza chembe chembe mpya, ikipunguza mashambulizi ya virus au kuzuia kabisa.

Dawa hiyo imeundwa kwa ajili ya watu ambao hawajaambukizwa bado virus ili kujilinda.

Watu zaidi ya milioni 1.1 nchini Marekani wanaishi na VVU, huku mmoja kati ya saba wakiwa hawana habari kama wameambukizwa.

Kwa sasa, hakuna tiba ya VVU bali kuna dawa za kufubaza makali ya virusi maarufu  ARVs lakini mara nyingi vinasababisha kichefuchefu, kutapika na usingizi.

Matokeo ya chanjo yamekuja huku maofisa wa afya wakibainisha Novemba mwaka jana kuwa janga la VVU linazidi kukua kwa kasi kwa maambukizo kufikia kiwango cha juu mwaka 2016 tangu rekodi zianze kuchukuliwa.

Mwaka 2016, watu 160,000 waliambikizwa VVU katika nchi 53 za Ulaya, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha udhibiti na Uzuuiaji wa Maradhi Ulaya.

Kipindi cha mwongo uliopita,  kiwango kipya cha maambukizo mapya ya VVU Ulaya kilipanda kwa asilimia 52 kutoka asilimia 12 kwa kila watu 100,000 mwaka 2007 hadi asilimia 18.2 kwa kila watu  100,000 mwaka 2016, utafiti unaongeza.

Kwa mujibu wa ripoti, ongezeko hilo limechochewa zaidi na kuendelea kwa maambukizo mashariki mwa Ulaya, ambako kunachukua asilimia 80 ya kesi zote za maradhi hayo Ulaya.

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Ulaya, Zsuzsanna Jakab, awali alisema: “Hii ni idadi ya juu ya kesi zilizorekodiwa kwa mwaka mmoja. Iwapo mwelekeo huu utaendelea hivi, hatutaweza kufikia lengo la kuhitimisha VVU ifikapo mwaka 2030.”

Matokeo ya nyuma yanaeleza kuwa viwango vya maambukizo ya VVU vilipanda mashariki mwa Ulaya hasa kwa wale wenye umri wa miaka zaidi ya 50 wanaojidunga dawa haramu za kulevya.

Hilo linadhaniwa ni kutokana na ukosefu wa kampeni za uelewa kuhusu hatari za maambukizi na namna ya kuzuia kuenea kwa VVU.

Pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha maambukizo ya VVU barani Ulaya, takwimu zilizotolewa Julai mwaka jana zinaonesha vifo vinavyohusiana na Ukimwi vimepunguzwa kufikia nusu kipindi cha miaka 10.

Idadi ya vifo kutokana na VVU duniani ilipungua hadi milioni moja mwaka 2016 kutoka milioni 1.9 mwaka 2005, kwa mujibu wa ripoti ya pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabili VVU/UKIMWI (UNAids).

Ripoti inasema kuwa idadi ya vifo imepunguzwa zaidi ya nusu kutokana na wagonjwa kutumia tiba za kufubaza makali ya VVU.

Lengo lililopo limelenga dawa kuwafikia watu milioni 30 ifikapo mwaka 2020.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mashariki na kusini mwa Afrika kunaongoza kama mfano mzuri wa kupungua kwa kesi za maambukizo mapya ya VVU kwa karibu theluthi moja tangu mwaka 2010.

UNAids imeweka mkakati ujulikanao ’90-90-90′ ambao kufikia mwaka 2020 umelenga asilimia 90 ya wanaoishi na VVU kujitambua hali zao, asilimia 90 kupata tiba na asilimia 90 maambukizo kutokomezwa.

Mwaka 2016 tawimu hizo zilikuwa asilimia 70, 77 na 82.

 

Kwanini dawa ya kutibu VVU bado haijapatikana?

Wakati kukiwa na matumaini ya kupatikana chanjo ya kuzuia maambukizi kama utafiti mpya ulivyojieleza, tiba ya ugonjwa huo bado changamoto ingawa wanasayansi mara kadhaa wameeleza matumaini.

Sababu kuu inayozuia upatikanaji wa tiba itakayoweza kuviua kabisa virus hivyo au upatikanaji wa kinga ya kuvizuia kuingia kwenye mwili na kuleta madhara ni uwezo wake mkubwa wa kubadilika na kujenga kuta zinazozuia dawa isiweze kufanya kazi ya kuvidhuru.

Uwezo huo wa VVU, umekuwa changamoto kubwa inayozuia dawa zote zilizowahi kutengenezwa kwa ajili ya kuviua kushindwa kufanya kazi hiyo.

Naam, wanachofanikiwa watafiti wengi katika majaribio yao ni kuviondoa virus kutoka damu, lakini baada ya muda wanakuta vimerudi.

Ni hapo katika uchunguzi wao walikuja baini kuwa seli za VVU zina tabia hiyo ya kujificha ficha.

Miongoni mwa maeneo vinakopenda kujificha ni pamoja na katika ubongo, uti wa mgongo, utumbo na kadhalika.

Hivyo wanasayansi mkazo umekuwa sasa kuangalia namna ya kuviamsha va kuvivuta virus hivyo kutoka mafichoni na kujitokeza sehemu ya wazi kwa ajili ya kuangamizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles