27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

AIBU KUENDELEA KUSHUHUDIA TUZO ZA WENZETU ZIKISTAWI

 

NA MWANDISHI WETU

MAPEMA wiki hii uongozi wa tuzo za All Africa Music Awards (AFRIMA 2017) za huko nchini Nigeria ulitoa orodha ya wasanii mbalimbali wa bara la Afrika waliochaguliwa kuwania vipengele mbalimbali vya tuzo hizo kwa mwaka huu.

Tuzo hizo, ambazo huwatunuku wasanii kutokana na ubora na uzuri wa nyimbo zao, zimevutiwa na kazi za wanamuziki watano wa Bongo Fleva, ambao ni Diamond Platnumz (Eneka), Ali Kiba (Aje), Lady Jay Dee (Sawa Nao), Vanessa Mdee (Cash Madam) na Nandy ameingia kwenye AFRIMA mwaka huu kupitia wimbo wake wa One Day.

Tuzo za AFRIMA safari hii zitatolewa Novemba 10-12, jijini Lagos na kila mwaka huwa zinatolewa zikiambatana na zile za AFRIMMA za kule Marekani, ambazo wiki chache zilizopita nazo zilitangaza wasanii ambao wanawania, huku Bongo Fleva nayo imetoa wasanii wake kwenye vipengele tofauti tofauti vya tuzo hizo.

Mwaka huu pia msanii Ray Vanny ameibuka kidedea kwa kushinda tuzo kubwa dunia za Black Entertainment (BET) huko Marekani. Ukishaona kuna mfululizo wa tuzo kutoka nje ya nchi zinaona uwezo wa wasanii wetu na kuwaweka kwenye tuzo zao, basi ujue tasnia inakua.

Hivyo basi, tunahitaji kuwa na tuzo zetu ambazo zitaongeza ushindani kwa wasanii wa ndani, kabla ya kukabiliana na wasanii wenzao wa mataifa mengine, ikumbukwe kuwa tuzo ni kitu muhimu mno kwa uhai wa muziki wetu, ndiyo maana ukiangalia hizo tuzo tunazoziita za kimataifa zinafanyika kila mwaka.

Mbali na kufanyika kila mwaka, tuzo za wenzetu zimeendelea kuboresha vipengele vya tuzo, hivyo kufanya ziendelee kuwa bora na kujijengea heshima zaidi. Binafsi huwa naona aibu kuendelea kushuhudia tuzo za nje ya nchi zikiendelea kufanya vizuri, huku hapa nyumbani kukiwa kimya.

Ni miaka isiyopungua miwili sasa Tanzania hatuna tuzo kuu za muziki. Ukiacha zile zinazoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ambazo ndiyo tulikuwa tunazitegemea, hata nyingine ambazo zimeanzishwa bado hazitoshi kipindi hiki ambacho tunahitaji ushindani wa ndani wenye tija.

Inachosha kuona wasanii wetu wakitajwa kuwania tuzo za wenzetu wakati, sisi hapa nyumbani ni patupu. Nadhani wadau wanaohusika na haya masuala wanaweza kuona namna nzuri zaidi ya kuzirejesha tuzo za ndani ili twende sawa na maendeleo ya sasa wa muziki.

NUKUU

“Mafanikio siyo pesa, mafanikio ni kuwa na watu na ukaishi nao vizuri, maana pesa hata siku ukidondoka haziwezi kukuokota hadi uite watu.”

Diamond Platnumz.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles