31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TUKATAE KUJENGA TAIFA LA WAVIVU

 

SHERIA ya kwanza ya mwanasayansi Isaac Newton kuhusu mwendo inasema hivi:

“An object at rest stays at rest and an object in motion stays in motion with the same speed and in the same direction, unless acted upon by an unbalanced force”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi kwa lugha ya Kiswahili ni kwamba; kama kitu kipo mahali fulani kitaendelea kuwa pale na kama kipo kwenye mwendo kitaendelea kuwa kwenye mwendo ule ule na mwelekeo ule ule hadi pale itakapotokea nguvu fulani ya kukizuia.

Sheria hii inaweza kuwa na maana kubwa katika maisha yetu, kwamba ukiamua kukaa bila kusumbua akili yako kutafuta kitu cha kufanya, utaendelea kubaki hivyo hivyo na kama ukiamua kufanya jambo la maendeleo pamoja na changamoto utakazokutana nazo usipokata tamaa, ni wazi utajifunza, utafikiri zaidi na hata kusonga mbele.

Tumelazimika kuzungumzia haya kutokana na ukweli kwamba, miongoni mwetu wengi tumejenga hulka ya uvivu pasipo kujua kwamba tunatengeneza bomu la hatari katika Taifa letu.

Uvivu maana yake ni kutokuwa tayari kufanya kazi au kutumia nguvu zetu, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema mara nyingi hii hutokea kutokana na mawazo yetu potofu au mabaya.

Kwa upande wa dini zetu, tabia ya uvivu ni dhambi na ndiyo maana watu wenye tabia hizi wengi wao, si wote, mara nyingi huishia kuvuta dawa za kulevya, kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu n.k kwa sababu ya uvivu hukusababisha ushindwe kufanya vitu vya muhimu unavyovihitaji katika maisha.

Leo hii na hasa nyakati za masika si ajabu ukapita katika maeneo fulani ya nchi (si yote bali mikoa fulani fulani), licha ya kubarikiwa kuwa na ardhi nzuri, ukashangaa kuona mashamba yao hayajalimwa wala kupandwa chochote, ukiuliza kisa utaambiwa wametingwa kuvua samaki.

Si hilo tu, kuongezeka kwa wimbi la vijana wenye elimu na wasio na elimu katika vijiwe mbalimbali na hata kujiingiza katika matendo yasiyofaa, hili nalo limebeba sura tofauti.

Licha ya serikali kwa upande wake kushutumiwa kutokuwa na mipango bora ya kuwapatia ajira, lakini vijana nao kuogopa kutumia fursa zilizopo kwa sababu tu haziendani na hadhi zao za kielimu, ni tatizo jingine ambalo limezama kwenye hulka hii.

Tangu Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani, amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kukerwa na kitu kinachoitwa uvivu.

Mara kadhaa Rais Magufuli amekaririwa akisema kuwa, katika utawala wake hakutakuwa na vitu vya bure.

Kwamba wakati wa kukaa kwenye magenge na kupiga maneno umepita.

Pamoja na kwamba kauli kama hizo zimekuwa kikiwakera baadhi, lakini huo ndio ukweli mchungu tusioupenda kuusikia baadhi yetu.

Kwa sababu hiyo, sisi tunaona yapo ambayo yanapaswa kufanywa na serikali ili kuwaondoa watu katika dimbwi hili la uvivu, kama kutengeneza ajira na fursa ambazo zitawapatia kipato wananchi wake.

Lakini kwa upande wa kila mmoja wetu, tunapaswa kukataa tabia hii, na msingi wa kwanza ni kubadili fikra zetu, tukifanya hivyo tutaweza kuona fursa zilizopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles