28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

WENYE MZIGO WA VIROBA WALETE BARUA -RC

Na BEATRICE MOSSES- MANYARA

MKUU wa Mkoa  wa Manyara, Dk. Joel Bendera, amewataka  wafanyabiashara wote wenye shehena kubwa ya viroba kuandika barua kwa Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais kuomba kibali cha (re-parking) ili waweze kuuza kwa utaratibu uliowekwa na Serikali.

Aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa wanachama wote wa TCCIA Mkoa wa Manyara, uliofunguliwa jana  katika ukumbi wa ‘White Rose’ mjini Babati ambapo alisema  kero hiyo ya wafanyabiashara imepata ufumbuzi baada ya Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa ufafanuzi.

Alisema amepokea maagizo kutoka kwa  Waziri wa Viwanda na Biashara ya kuwataka wafanyabiashara kuandika barua ya kuomba vibali vya kuuza tena shehena zao za viroba  walivyokuwa wamenunua kabla ya Serikali haijapiga marufuku uingizaji na uuzaji.

“Natamka kuwa nimepata maagizo kwa wafanyabiashara wote  wenye shehena za viroba muandike barua ya kuelezea idadi kamili ya viroba ulivyonavyo na andika barua eleza una kiasi gani kama una godaoni zima, eleza kiasi ulichokuwanacho halafu omba  kwamba naomba utaratibu wa kure-parking ili ushughulikiwe, wizara inatoa vibali na wanakuruhusu na ikiwezekana hizo barua zipitie TCCIA Manyara na nakala ofisi ya mkuu wa mkoa,” alisema Bendera.

Aidha, aliwaomba viongozi wa Chemba kwa kushirikiana na Serikali  kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi  kuhusu ulipaji wa kodi na tozo nyingine  kwani kwa kufanya hivyo kutaharakisha uletaji wa maendeleo kwa wananchi na kutasaidia kutekeleza maagizo ya Rais Dk. John Magufuli ya uanzishwaji wa viwanda.

Alieleza kwamba, TCCIA Manyara ina wajibu wa kutoa huduma stahiki kwa wanachama wake na wajasiriamali ikiwa ni pamoja na makundi maalumu ya vijana na wanawake  kwa kuwa na miradi midogo midogo  kwa makundi hayo kama vile mabwawa ya samaki, kilimo cha mboga mboga na ufugaji wa kuku.

“Hata katika maonyesho ya wakulima na wafugaji Nanenane, wamekuwa wakipelekwa wataalamu pekee pasipo kuguswa makundi ya wanawake na vijana ambao ndio walengwa hivyo utaalamu huo unabaki kwa wataalamu pekee badala ya watu wa chini,” alisema Bendera.

Naye Makamu wa Rais wa TCCIA Taifa, Octavian Mshiu,  akimwakilisha Rais wa TCCIA, aliomba Serikali ya Mkoa kutenga eneo la viwanda litakalouzwa kwa bei nafuu kwa wafanyabiashara ili waweze kujenga viwanda vitakavyoongeza ajira na kutii agizo la Rais la uanzishwaji wa viwanda nchini.

Pia aliomba urasimishaji wa biashara kwa kuwa wafanyabiashara wengi  wadogo na wakubwa waliopo mkoani Manyara hawajaandikishwa kisheria  na hawatambuliki serikalini  kwa kuwa bajeti ya mwaka huu Serikali imekubali kuwatambua wafanyabiashara ndogo ndogo.

“Ili wafanyabiashara ndogo ndogo waweze kutambulika na Serikali ni lazima wasajiliwe  na waweze kupewa TIN namba kwa kuwa moja ya jukumu la Chemba ya Biashara ni kusajili wafanyabiashara  ili waweze kulipa kodi kwa hiari,” alisisitiza Mshiu.

Alishauri Mkoa wa Manyara kupewa kipaumbele cha pekee  katika  kutoa maeneo ya kujenga mahoteli makubwa ya uwekezaji  katika utalii kutika Hifadhi ya Ziwa Manyara  na Ziwa Babati  ni maeneo yenye vivutio vya kujenga   mahoteli makubwa kwa ajili ya watalii na kujenga kiwanda cha kuchakata, kupolishi na kukata  madini ya Tanzanite Mirerani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TCCIA  Manyara, Stanley Mchome,  alisema tangu kuanzishwa kwa Chemba ya Biashara mwaka 2004  imewezesha  kuongeza idadi ya wanachama kutoka 93 hadi 877 na kuanzisha matawi katika wilaya zote za mkoa  huo pamoja  na kufanya mabaraza ya wilaya na mkoa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles