Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
TAASISIi mbalimbali za Serikali zimekutana Dodoma kufanya mazungumzo ya awali kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuwa pikipiki zote zinazotumika kusafirisha abiria zifungwe tela, ikiwa ni mkakati wa kupunguza ajali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu alikuwa akizungumza jijini hapa jana wakati wa maonyesho ya pikipiki ya mfano yenye tela zinazotengenezwa na Shirika la Mzinga.
Alisema serikali imedhamiria kuondoa na kukomesha ajali za bodaboda na kulinda usalama wa watumiaji wa usafiri huo.
Alisema wizara yake kwa kushirikiana na wadau wengine kutoka taasisi za serikali, Shirika la Mzinga, Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi(Veta), Shirika la Viwango Tanzania(TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(Sido), Kiwanda cha Kutengeneza Magari (Nnyumbu) na Jeshi la Polisi zitahakikisha zinakuwa na mpango wa pamoja wa kuratibu na kuhakikisha mkakati huo utakaosaidia kupunguza ajali unakamilika.
“Leo (jana) tumekutana hapa kujadili jinsi ya kuliendea jambo hili la kufunga tela.
“Kamati ya wataalamu hawa ndiyo itakutana na kuratibu andiko ambalo litapelekwa kwa viongozi wa wizara mbalimbali zinazohusika na suala la kudhibiti ajali za barabarani na kumlinda mtumiaji wa huduma ya usafiri huo,” alisema Meja Jenerali Kingu.
Aliwataka wananchi wawe na subira kipindi hiki ambacho kamati hiyo ya wataalamu inaenda kuandaa mpango huo na mapema mwishoni mwa mwaka huu mpango huo utatangazwa .
Akizungumzia pikipiki hiyo ya mfano yenye tela, Mtaalamu kutoka Shirika la Mzinga, Salum Kipande alisema pikipiki hiyo imetengenezwa vizuri na itakua na uwezo wa kubeba abiria wanne na dereva mmoja.
Mtaalamu huyo alisema wanaendelea kuunga mkono azma ya serikali kupunguza ajali za bodaboda nchini kwa kutengeneza pikipiki hizo kwa ustadi.
Kaimu Mkurugenzi Elimu na Mafunzo wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Stella Ndimubenya, alisema wao kama VETA watahakikisha wanatumia teknolojia waliyonayo kuweka kifaa maalumu ambacho kitadhibiti upakiaji wa abiria kupita kiwango.