Amina Omari na Oscar Assenga, Korogwe
VYOMBO vya ulinzi mkoani Tanga vimeanza kuchukua hatua ya agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwataka kudhibiti tatizo la uingizaji wa dawa za kulevya, baada ya kufanikiwa kukamata viroba vya mirungi 12 vyenye uzito wa kilo 212 vikiwa vinasafirishwa.
Wafanyabiashara hao walikamatwa juzi saa 9:30 alasiri katika kizuizi kilichopo Kwasunga, Kata ya Makuyuni, wakiwa na lori lenye namba za usajili T620 BVR na tela lenye namba za usajili T749 BSN aina ya mali ya Kampuni ya Ladhia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watuhumiwa hao kuwa ni dereva wa gari hilo, Juma Hassan mkazi wa Arusha, utingo wake Hassan Juma na Husein Abubakari, fundi magari mkazi wa Arusha.
Alisema watuhumiwa wote wanashikiliwa na polisi huku upelelezi kuhusu tukio ukiendelea.
Katika tukio jingine, jeshi hilo linamtafuta mkazi wa Kilindi, Hilal Yohana, kwa kosa kumkata miguu mkulima Parandi Magile akiwa shambani.
Alisema tukio hilo limetokea Julai 13, mwaka huu, saa 2 asubuhi katika eneo la kitongoji cha Mchenjeuke, kilichopo Tarafa ya Mswaki.
Hata hivyo, Magile alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilindi, huku chanzo cha mauaji hayo kikiwa bado hakijulikani.