24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya IPTL haitakufa – Kafulila

David Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila

Na Charles Mullinda, Dar es Salaam

SIKU moja baada ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kumfungulia kesi ya madai Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kwa kuichafua na kutoa taarifa za uongo kwa umma ikimdai fidia ya Sh bilioni 310, ameibuka na kudai kuwa kashfa hiyo haitakufa hata kama atafungwa jela.

Amesema anao ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha tuhuma alizozitoa kuhusu kuwepo kwa mchezo mchafu ndani ya IPTL, taifa kupoteza mabilioni ya fedha kutokana na ufisadi ilioigubika kampuni hiyo na jinsi viongozi wa juu wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoufumbia macho.

Akizungumza na MTANZANIA jana kupitia simu yake ya kiganjani kutokea Kigoma alikosema yuko katika ziara ya kuelimisha umma kuhusu mchezo mchafu uliohusisha vigogo wa Serikali na Kampuni za IPTL na PAP, aliodai uliziwezesha kupora Sh bilioni 200 zilizokuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Escrow, Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kafulila alisema amesikia taarifa za kufunguliwa kwake kesi ya madai kupitia vyombo vya habari, lakini hajafikishiwa rasmi.

Alisema anashangazwa na hatua hiyo na kuhoji mamlaka za nchi zinahitaji ushahidi wa aina gani ili kuchukua hatua hata baada ya yeye kusimama bungeni na kueleza kile alichokiita uchafu uliofanywa na kampuni hizo, kisha kuendelea kupigia kelele jambo hilo hata akiwa nje ya Bunge.

“Nimesikia magazetini kuwa nimefunguliwa kesi na Kampuni ya PAP inayodai kumiliki IPTL, kwamba nimewachafua ndani na nje ya Bunge. Watanzania waelewe kuwa hata wasio na haki wanao ujasiri wa kushtaki, ndiyo maana Yesu na hata Nyerere (Julius) walishtakiwa hivyo sishangai.

“Nasisitiza IPTL ni mfululizo wa ufisadi tangu ilipoingia na imeendelea kuwa fisadi hadi mwaka 2013 kwenye utoaji wa fedha za Escrow ambazo ni za umma. Najiuliza, nchi hii inahitaji vielelezo kiasi gani kusimama ndani na nje ya Bunge na kusema mchezo mzima wa IPTL ni mchafu (was dirty deal)?” alisema Kafulila.

Akifafanua kauli yake hiyo, alisema hukumu ya mwaka 2001 ya mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya kiuwekezaji ya kimataifa (ICSID), iliitia hatiani Kampuni ya IPTL kwa kudanganya kuhusu aina ya mitambo yake na kuipa ushindi Tanzania.

Kwamba katika hukumu hiyo, iliamriwa gharama ambazo IPTL ilikuwa ikilipwa bila kujali kama imezalisha umeme au la, (Capacity chargers) zishuke kutoka dola za Kimarekani milioni 4.2 hadi 2.6 kwa mwezi.

Akizungumzia kile alichokiita madudu aliyoyagundua ndani ya kampuni hizo katika uchunguzi wake wa kibunge, alisema ukaguzi uliofanyika ulibaini kuwa PAP ilidanganya kuwa ina mtaji wa dola za Kimarekani milioni 38 mkononi, ambayo ni sawa na asilimia 30 ya mtaji na kwamba asilimia 70 ilikuwa ni mkopo.

Alisema kinyume chake, ukaguzi ulibaini kuwa mtaji katika mradi wote ulikuwa ni mkopo na kwamba udanganyifu huo ulilenga kulipa mzigo Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO.)

“Tunapunjwa zaidi ya laki 7.8 kwa mwezi kwa gharama za capacity chargers tu, kwa mkataba huu wa IPTL wa miaka 20 maana yake taifa limepoteza na litapoteza Sh bilioni 300 kwa uhai wa mkataba. Hili liko wazi na ushahidi uko wazi kwa umma. Inawezekanaje hawa mafisadi watuibie na watukate tusikasirike?

“Upo ushahidi wa kutosha wa mpango mzima wa kupora dola za Kimarekani milioni 270 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 400 kwa kuanzia na kwa sasa tayari wamepora bilioni 200 ambapo Kampuni ya PAP/IPTL kwa kushirikiana na vigogo wa serikali wamefanikisha ufisadi huo, huku wakivunja sheria na taratibu za nchi,” alisema Kafulila.

Alieleza zaidi kuwa madai aliyoyatoa kuhusu kashfa hiyo siyo mapya, kwa sababu waliohusika na kashfa ya IPTL katika awamu tofauti za uongozi wanajulikana katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Usalama wa Taifa na Ikulu.

Alisema ofisi hizo zinao ushahidi wa kutosha kuhusu wahusika wa sakata hilo pamoja na majina yao, lakini katika hatua ya kushangaza taasisi hizo zimeshindwa kuwachukulia hatua wahusika kwa kuwafikisha mbele ya mikono ya sheria.

“Ndiyo maana nilitaka Kamati Teule ya Bunge ifanyie kazi jambo hili au kampuni za kimataifa za ukaguzi kama ilivyokuwa katika sakata la EPA, kwani vyombo vyetu havina uwezo wa kutosha katika jambo hili na hata wakichunguza ripoti zitachakachukuliwa tu kama ilivyofanyika katika historia ya ufisadi kwenye jambo hili kuanzia mwanzo.

“Nasisitiza mchezo mzima wa PAP na IPTL na uporaji wote wa fedha ndani ya Escrow akaunti ni mchezo mchafu na lazima watu watafungwa, hata kama siyo awamu hii kwa sababu ukweli huu unaishi na kuna siku tutapata rais asiyevumilia uchafu atafukua hata makaburi yao kama watakuwa wamekufa,” alisema Kafulila.

Kafulila amefunguliwa kesi ya madai namba 13 ya mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na wadai ni IPTL/PAP na Harbinder Sigh Seth, kupitia wakili Augustine Kusalika.

Wadai wanamdai Kafulila awalipe fidia ya Sh bilioni 210 kwa kutoa taarifa za uongo zilizochafua kampuni hiyo na awalipe shilingi bilioni 100 kama fidia ya jumla kwa usumbufu aliowasababishia kutokana na taarifa hizo.

Inadaiwa hakuna ubishi kwamba VIP Engineering and Marketing Limited na TANESCO waliweka benki Sh bilioni 200 katika akaunti ya Escrow wakisubiri kesi inayoendelea mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ndugu yangu Kafulila Mungu atakutetea, hawa mafisadi wana mwisho wao ndio maana walianza kutukana ovyo na kuwaita watu washenzi, lakini mwisho wao hauko mbali, haiwezekani wakaendelea kufanya uchafu huu nasi watanzania tukitazama tu. Songa mbele, tunakuombea, Ubarikiwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles