28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

AG Zanzibar azua tafrani

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman, jana alitibua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, baada ya kuikataa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Baada ya kupiga kura ya hapana, baadhi ya wajumbe walimzomea mwanasheria huyo wakionyesha kutoridhishwa na msimamo wake.

Kutokana na hali hiyo, baada ya Bunge kuahirishwa saa nne asubuhi, askari wa Bunge walilazimika kumtoa bungeni chini ya ulinzi mkali kwa kutumia mlango anaotumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingia bungeni.

Kabla walinzi hao hawajamfuata mwanasheria huyo, awali baada ya Bunge kuahirishwa jana, alikuwa akizungumza na wajumbe mbalimbali huku akionyesha atatoka katika ukumbi wa Bunge kupitia mlango wa kawaida wanaotumia wajumbe wote.

Wakati akijiandaa kuanza kutoka ukumbini huku akiendelea kuzungumza na wenzake, askari mmoja wa kike wa Bunge aliyeongozana na wenzake watatu ambao ni wanaume, alimfuata na kumnong’oneza jambo.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyodumu kwa sekunde kadhaa, askari hao waliongozana naye na kumpitisha katika mlango anaotumia Waziri Mkuu huku baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wakisema; “msaliti huyo”, “Ukawa huyo”, “huyo siyo kamanda anakimbia vita”.

Pamoja na kupitishwa katika mlango huo, askari hao hawakumtoa nje mapema, badala yake walikaa naye katika moja ya vyumba vya Bunge kwa zaidi ya nusu saa kwa kile kilichodhaniwa kuwa ni kuhofia usalama wake.

Baada ya muda huo kupita, AG Othman alitolewa nje akiongozana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, Makamu wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine wa Zanzibar.

Baada ya kutoka nje ya ukumbi akiwa chini ya ulinzi mkali uliokuwa umewahusisha askari wanne wa Kikosi Maalumu cha Kutuliza Ghasia (FFU), walipofika jirani na yanakoegeshwa magari yanayokuwa katika msafara wa Waziri Mkuu, yeye na Kificho walipanda kwenye gari lenye namba za usajili SMZ 6197 na kuondoka kupitia lango la viongozi wakuu wa Serikali.

Kabla ya tukio hilo, awali wakati Bunge linaendelea, Katibu wa Bunge aliita jina la Othman ili akapige kura kwa kuwa alikuwa hajafanya hivyo tangu upigaji kura ulipoanza siku mbili zilizopita.

Mwanasheria huyo alipoitwa jina lake, alisimama na kusema atapiga kura ya wazi, na kwamba hakubaliani na baadhi ya ibara zilizo katika rasimu hiyo.

Alianza kwa kuigusia sura ya kwanza na kuzitaja ibara asizokubaliana nazo kuwa ni ibara ya pili inayohusu eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya tisa inayosema Katiba ni sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba na pia aliikataa ibara ya 86 inayohusu uchaguzi wa rais iliyoko katika sura ya nane.

Othman aliitaja sura ya saba na kuzikataa ibara za 70 hadi 75 ambazo zinahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano ambazo msingi mkuu wa ibara hizo ni muundo wa Serikali mbili.

Alizikataa pia ibara za 128 na 129 zilizoko katika sura ya kumi ambazo zinaeleza muundo wa madaraka ya Bunge.

Baada ya kuzitaja ibara hizo, aliitaja sura ya 11 na kuzikataa ibara za 158, 159, 160 na ibara ya 161. Sura hiyo inazungumzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Aliigusia pia sura ya 10 na kuzikataa ibara za kuanzia 142 hadi 151 zinazohusu uongozi wa Bunge, kisha akaikataa nyongeza ya kwanza iliyoko katika ibara ya 70.

Baada ya mwanasheria huyo kumaliza kupiga kura yake, baadhi ya wajumbe walianza kutoa maoni yao juu ya msimamo wake huo na aliyekuwa wa kwanza kumjadii ni Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim (CCM).

Yahya alisema anashangazwa na uamuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa kuikataa rasimu wakati hakushiriki mijadala yake.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tulioko humu tumepiga kura kwa sababu tulishiriki kujadili rasimu, lakini huyu Mwanasheria wa Zanzibar amepiga kura wakati hakushiriki mjadala.

“Hakushiriki mjadala si kwa sababu anaumwa bali ni kwa sababu ya kejeli na jeuri yake tu kutuonyesha kwamba amesoma. Sisi tulitegemea awepo hapa tangu mwanzo kwa sababu Rais wa Zanzibar alimteua ili awe msaidizi wake, lakini hamsaidii.

“Hivi mwanasheria kama huyu ana masilahi gani na Wazanzibari, yaani rais amemteua amsaidie halafu yeye anatoroka, hivi unaweza kutwambia nini juu ya mtu kama huyu?” alisema Kassim.

Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, alisema kanuni za Bunge haziruhusu kuzungumzia uamuzi wa mtu, hivyo akataka wajumbe waheshimu uamuzi wake.

Hivi karibuni, Othman alijitoa katika Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni baada ya kamati hiyo kuzikataa hoja 17 alizotaka ziwekwe katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Hata hivyo, wakati Balozi Idd akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa hivi karibuni, alisema hoja za Othman ambazo hazikukubaliwa ni nne lakini bado zinafanyiwa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles