24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

…Ukimya matokeo ya kura, Sitta alia na maaskofu

NA MAREGESI PAUL, DODOMA

KUCHELEWESHWA kutangazwa kwa matokeo ya kura za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, kumezua maswali mengi.

Msingi wa maswali hayo unatokana na uchache wa wajumbe wa Bunge hilo, kulinganisha na kura za madiwani ama wabunge ambazo zikipigwa matokeo yake huanza kutoka siku hiyohiyo.

Bunge Maalumu la Katiba lina wajumbe 629, kati yao 419 ni kutoka Tanzania Bara na 210 upande wa Zanzibar.

Katika kura zilizopigwa juzi, sehemu kubwa ya wajumbe walipiga kura za wazi huku wachache wakipiga za siri.

Katika siku hiyo ya upigaji kura, wajumbe waliokuwapo kwa upande wa Tanzania Bara ni 295 huku wale wa kutoka Zanzibar wakiwa 142.

Wajumbe waliopiga kura za wazi za ndiyo kutoka Zanzibar walikuwa takribani 136 huku upande wa bara wakiwa 295 wakati za hapana kutoka Zanzibar walikuwa takribani saba. Wajumbe wengine ambao hawapo ndani ya Bunge hilo wanaotarajiwa kupiga kura walikuwa ni chini ya 10.

Kutokana na idadi hiyo ndogo ya wajumbe na ukweli ambao ulishaonekana wa wajumbe waliopiga kura za ndiyo na hapana, ilitarajiwa matokeo yangetangazwa jana asubuhi, kitu ambacho hakikufanyika.

Pia suala la kuundwa kwa Kamati ya Maridhiano ambalo wengi walilitafsiri kama kubadilisha mtazamo wa waliopiga kura ya hapana, linaendelea kuzua maswali.

KUNYIMWA KUPIGA KURA

Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, akizungumza bungeni jana asubuhi, alitoa ufafanuzi wa mjumbe aliyelalamika kunyimwa kupiga kura akiambiwa asubiri Kamati ya Maridhiano.

Katika hali ya kushangaza, mwenyekiti huyo alisema alichukua uamuzi huo baada ya mwenyekiti wa chama cha siasa ambacho mjumbe huyo anatoka, kumweleza kuwa mjumbe huyo alipiga kura ya hapana kwa sababu hakuelewa.

“Jana mjumbe mmoja anaitwa Mwanaidi aliniandikia ujumbe, eti jina lake lilirukwa kwahiyo anataka apige kura.

“Lakini, Mwenyekiti wake wa chama ambacho ni NRA, aliniambia mjumbe huyo alikuwa amepiga kura ya hapana kwa sababu alikuwa hakuelewa maana yake.

“Hivyo, mwenyekiti huyo kaniandikia asipige kura, sasa katika mazingira kama hayo, lazima pawepo na mashauriano kwa ajili ya kumwelewesha.

“Kwa mfano, unakataa hata haki ya kuishi, kwahiyo kutokana na rai ya mwenyekiti wa chama hicho, nikamjibu mjumbe huyo apige kura baada ya mashauriano,” alisema.

WAJUMBE KUTISHWA

Katika hatua nyingine, Sitta alisema juzi walilazimika kutumia vyombo vya dola kumnusuru mjumbe mmoja aliyekuwa amezuiwa katika nyumba moja ili asipige kura.

Sitta alitoa taarifa hiyo bungeni jana alipokuwa akihitimisha upigaji kura kwa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ulioanza juzi.

“Kuna baadhi ya watu wasioutakia mema mchakato huu ufike pazuri kwa sababu watu hao wanawafungia wajumbe ndani ili wasipige kura.

“Kwa mfano, jana ilibidi tutumie mamlaka ya usalama kumkomboa mjumbe mmoja aliyefungiwa mahali fulani ili asipige kura, lakini baada ya kumkomboa, alikuja kupiga kura.

“Jamani, kumfungia mtu ni kosa la jinai, kama kuna watu hawataki mchakato huu, watumie njia halali. Kuna wengine jana walifika kwa katibu wakaonyesha ujumbe wa vitisho na kwa kuwa waliogopa, tuliwaruhusu waondoke.

“Hivi Watanzania mnaochukia mchakato huu na kulazimika kutumia mbinu za jinai mnataka nini hasa? Mimi naamini hawaitakii mema nchi hii.

“Pia, kuna mjumbe mwingine kutoka Zanzibar alikuwa akimshikilia mjumbe mwenzake kama mfungwa wake na amekuwa akifanya kazi ya kuhakikisha mjumbe huyo anapiga kura ya hapana.

“Hawa watu hawawezi kufanikiwa hata kidogo, hawa waliodhani wamepunguza kura za wenzetu wenye mwelekeo wa CUF, hawatashinda.

“Hebu ngoja niwape taarifa tu, kwamba baada ya tangazo langu, kuna wajumbe wawili kutoka nje waliokuwa wameweka mgomo, wamesoma rasimu wakaona ni kitu cha uzalendo, hivyo wakapiga kura.

“Nawaambia Mungu akitaka jambo litakuwa tu kwani hawa wawili waliokuwa wamesusa, mmoja akiwa tayari kufukuzwa katika chama, wamepiga kura.

“Watu hawa wanatumia mbinu za hovyo hovyo, ukiziba maji hapa, mkondo wa maji unaelekea kwingine, kwahiyo tusubiri matokeo tutayatangaza,” alisema Sitta.

SITTA NA MNYIKA

Katika hatua nyingine, Sitta amesema Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amemtukana wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara jijini Mwanza, hivi karibuni.

Pamoja na matusi hayo, alisema amemsamehe kwa sababu Mnyika ni kati ya vijana wanaojifunza siasa nchini.

“Kuna bwana mmoja anaitwa John Mnyika, huyu amenitukana mimi na Chenge (Andrew Chenge), ametuita sisi ni maharamia na ameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara kule Mwanza.

“Unajua taabu ya vijana hawa wametoka vyuoni majuzi, sasa wanadhani siasa ni mazingira kama ya kwenye vyuo, yaani uongozi wa chuo wanauleta katika medani za siasa, hii haiwezekani na kama wanajiandaa kuongoza nchi kwa kutumia mbinu za kichuo chuo, wajue wanapoteza muda.

“Wanapoteza muda kwani kadiri umma utakavyoendelea kuwaona kwamba hawajakomaa na wana mbinu za kitoto, wana kauli za hovyo hovyo, wajue hawataaminiwa.

“Wenyewe waendelee tu, lakini kusema watashika madaraka kwa kauli hizo huko ni kupoteza muda. Mimi namsamehe kwa sababu ni kijana mdogo, ndiyo anakomaa anaelekea kwenye utu uzima,” alisema.

Pamoja na hayo, Sitta alisema kimsingi Mnyika hakupaswa kumtukana kwa sababu umri wake ni mdogo ikilinganishwa na umri alionao yeye.

“Mimi ni kama baba yake, lakini kama anaona siwezi kuwa baba yake, basi aniheshimu kwa uzee wangu kwa sababu mimi ni kati ya wazee wa nchi hii,” alisema Sitta.

AWAVAA MAASKOFU

Pia Sitta alisema pamoja na uwapo wa nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kutolewa na maaskofu wasiotaka Bunge liendelee, yeye binafsi haamini kama wanaweza kutoa matamko hayo kwa kuwa hayana utukufu wowote.

“Naomba nimalizie na mababa zangu wa kiroho hawa maaskofu. Natuhumiwa kwenye blogs, kuwa nawadharau sana, sasa nasema kama wana matendo kama hayo, basi inabidi tuwadharau tu.

“Hapa ninao waraka ambao umelazimishwa kusomwa makanisani, lakini sioni utukufu ndani yake. Waraka huu unamwamuru rais arudishe Tume ya Katiba, hivi kwa maagizo hayo kuna Ukristo hapo?

“Waraka huu unamlazimisha rais asitishe mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, hivi tangu lini viongozi wa kidini wakatoa maagizo ya mambo ya siasa, hii si haki hata kidogo.

“Kwanza hata lugha iliyoandikwa humu ni ya wale tuliowazoea kama Ukawa, hivi kweli maaskofu wanaweza kusema Wizara ya Katiba na Sheria irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zikae zote humo ili wananchi waone kazi waliyofanya pamoja na kujifunza kwa na kujalidili rasimu kwa uwazi?

“Haya ni maelekezo ya kikristo kweli, kwamba Bunge Maalumu lijadili na kuboresha tu maoni yaliyo kwenye rasimu na si kufanya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1977, yaani wanapingana na hukumu ya mahakama ambayo imetoa uwanja mpana wa kujadili na kuona Katiba inakaa vizuri.

“Hawa wanataka mchakato usimamishwe ili kupisha maridhiano na mabadiliko yafanyike kwa uwazi, eti katika tamko hilo askofu anaweka kifungu cha kulinda rasimu ya pili, kweli hii ni sawa?

“Viongozi hao wanasema natumia ubabe, hivi hawa maaskofu wanaweza kusema natumia ubabe na kiburi wakati kuna wengine huko nje wanatutukukana, hivi hawawaoni hao?

“Watu wametutukana kwa maneno mangapi, yaani wengine mpaka wanaitisha press conference kututukana waziwazi, wanasema wajumbe wasitumie wingi wao wa CCM, hivi hii siyo siasa ni nini?

“Waraka wa maaskofu eti unasema kila mahali tume ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria na kujibu maswali ya Bunge Maalumu, wanataka eti tume ifufuliwe na tena wamenukuu kwenye vitabu vitakatifu kwenye Warumi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

 1. hahahahahahahahahaha!!!!!!!!!!!!!!! Mzee sita unazeeka vibaya tena unatapatapa si unaendeleza mchakato wa kura wasiwasi wa nini???

  Endelea na mchakato tuone km utashinda kwa nini unalialia??
  Umetukanwa wapi na nani? ulivyokua unaingi makanisani na kuzungumza mambo ya watu na ufisad mle ni mahala pake??? au umesahau mzee??

  wabaya wako wote ukiwaanika makanisani au umesahau kwanini leo maaskofu unasema wapo ktk siasa,Acha ukanjanja…

  VITA VYENU HAMTA SHINDA NA NCHI ITAKUWA NA AMANI MAISHA YOTE VIZAZI NA VIZAZI.

  WATZ OYEEEEEEE!!!!!! MALIZENI UPUUZI WENU SS TUUPIGE CHINI KTK KURA YA MAONI.

  HAhahahahahahaha hahahaha hahahaha SITA UNAZEEKA VIBAYA

 2. Mheshimiwa Samweli Sitta anapaswa kufahamu kuwa, katika kitu usichokitaka hata siku moja hutakiona kama kina utukufu ndani yake. Ndiyo maana bwana Sitta anasema haoni utukufu katika barua waliyoandika watu wa Mungu.

  Yesu Kristo pamoja na matukufu mengi aliyoyafanya wale ambao walikuwa hawamtaki walikuwa hawaoni matukufu hayo hata walifikia kumwua!.. Kwa jinsi hiyo hiyo, Samweli Sitta asingeweza kuuona na wala hatauona utukufu wowote kwa waraka huo wa watu wa Mungu kwa sababu yeye tayari yupo kinyume na waliouandika; yeye tayari ameshakuwa kinyume; atauonaje utukufu?

  Mungu tu atusaidie, Taifa letu kama tulivyojizoeza kuwa na amani na kuwa na hofu na magomvi, basi atusaidie tuwe hivyo. Vinginevyo mimi binafsi ninachoona mbele yetu ni matatizo matupu hakuna amani, hata Mheshimiwa Sitta mwenyewe anashuhudiwa hivyo, kwamba hali siyo nzuri hata kidogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles