28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

AG AIONYA MAHAKAMA KESI YA UCHAGUZI KENYA

NAIROBI, KENYA

MWANASHERIA Mkuu (AG) wa Kenya, Profesa Githu Muigai, ameionya Mahakama Kuu kutosukumwa na kelele za wanasiasa katika usimamizi wa kesi ya Uchaguzi Mkuu inayoendelea na badala yake wasimamie sheria.

Alisema katika baadhi ya kesi zilizopita majaji walishawishiwa kuziendesha kwa kutozingatia viwango vya sheria za nchi.

AG aliiomba mahakama hiyo kuangalia kwanza masilahi ya wapigakura badala ya vyama vya siasa au wanasiasa pekee.

“Waheshimiwa, uchaguzi si vyama vya kisiasa na wanasiasa, ni haki ya mpigakura. Mahakama inapaswa kujiuliza swali rahisi: Je, uchaguzi ulikuwa haki na huru? Je, kulikuwa wa uwazi, upendeleo, ufanisi, usahihi na uwajibikaji?” alisema.

Mwanasheria huyo alisema jibu la swali lolote kuhusu uchaguzi linaweza kupatikana katika katiba.

Hata hivyo, alisema si vema kutegemea katiba pekee kwa sababu imetoa mamlaka kwa Bunge kuanzisha sheria zinazoongoza mchakato wa uchaguzi.

Alisema mahakama haipaswi kutegemea kikamilifu katiba pekee, bali isome sheria nyingine zinazohusu uchaguzi.

 AONYA WANASHERIA

Aidha, AG huyo aliwaambia wanasheria kuwa katiba si amri ya uchaguzi, lakini ina kanuni zilizozingatiwa katika kuunda mfumo wa uchaguzi.

“Waheshimiwa, katiba haiwezi kutoa jibu sahihi kama uchaguzi ulifanyika vizuri au la,” alisema.

Kwa upande wake, mwanasheria Stephen Mwenesi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na hali mbaya kwa sababu wanachama wake walikuwa katika makundi ya kupingana wakati wa kuwasilisha maombi ya kesi hiyo.

Alisema Kalonzo Musyoka ambaye alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga na wajumbe wengine, wawakilishi wa Rais Uhuru Kenyatta na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ni wanachama wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

 ODINGA AOMBA MATOKEO YAFUTWE

Kwa upande wake, Odinga ameomba Mahakama Kuu kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 kwa sababu Kenyatta hakuchaguliwa kihalali.

Odinga aliiambia mahakama kwamba uchaguzi huo haukuendeshwa ipasavyo, kwamba ulifanywa kwa kukiuka masharti ya kikatiba na kisheria.

Alisema matokeo ya mwisho hayakutegemea utoaji matokeo ya kielektroniki au fomu za kawaida za 34A au 34B.

Odinga alisema Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, alishindwa kujibu maswali yaliyotokana na uendeshaji wa uchaguzi huo.

Mwanasheria wa upande wa muungano wa vyama vya upinzani wa NASA, Otiende Amollo,  aliiambia mahakama kwamba badala ya IEBC, Chebukati na Kenyatta kujibu maswali hayo, waliamua kuitikia kwa njia ambayo wao walitaka iwe, wakidai kuwa kulikuwa na unyanyasaji kwa watu wa Kenya.

“Ukweli wa suala hilo ni kwamba wanasheria wa Rais Kenyatta, Tume na Chebukati wameonyesha dharau mbele ya mahakama hii.

“Sheria inahitaji matokeo ya urais yaje bila mpangilio kutoka vituo vya kupigia kura. Lakini hii haikuwa hivyo na hawajatekeleza hili,” alisema.

Katika uwasilishaji hoja yake, Mshauri Mwandamizi wa NASA, Pherozee Nowrojee aliwahimiza IEBC kuelezea jinsi walivyotangaza matokeo bila fomu 34A na kuongeza huo ulikuwa uthibitisho kwamba hapakuwa na uhakiki.

Mahakama hiyo inaendelea kusikiliza kesi iliyowasilishwa na NASA, kupinga ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi huo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles