22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

AFYA YA LISSU YAIMARIKA, AWEKEWA CHUMA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


AFYA YA Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu inatarajiwa kuimarika zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji mfupa katika mguu wake wa kulia.

Kufanyika kwa upasuajai huo jana kumetajwa kuwa ni sehemu ya marekebisho yanayofanywa na madaktari wanaomtibu ili  kurekebisha mfupa wake uweze kuunga kwa haraka.

Tayari kwa nyakati tofauti Lissu amekuwa akionekana kwenye muonekano wenye matumaini baada ya picha kutoka nchini Ubelgiji anakotibiwa kumuonyesha akiwa amesimama katika mazingira tofauti kama sehemu ya mazoezi.

Akizungumza mjini hapa kuhusu hali ya Lissu, Msemaji wa familia, Wakili Alute Mughwai, alisema hali ya Lissu inaendelea na vizuri.

“Lissu alikwenda Ubelgij kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu ya viungolakini akiwa huko ikaonekana ulazima wa kufanyiwa upasuaji mwingine kwenye mguu wake.

“Anaendelea vizuri, kuhusu lini atarudi nyumbani bado hatujajua inategemea taarifa ya daktari wake baada ya kufanyiwa upasuaji mguu.

“Lakini ukiniuliza ninaweza kuwa wa kwanza kutaka arudi mapema Aprili,” alisema Wakili Mughwai.

Aidha, alisema upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio kwa muda wa saa mbili na kwamba itamchukua siku saba hadi 10 akiwa amelazwa wodini.

ALIA NA UPEPELEZI

Kuhusu upelelezi wa tukio la kujeruhiwa kwake alisema mpaka sasa hakuna taarifa yeyote waliyopewa.

“Hakuna taarifa tuliyopewa kama ndugu licha ya kuziomba mamlaka ziombe msaada wa kiupelelezi kutoka nje, lakini tulijibiwa polisi wanaweza kufanya uchunguzi japo mpaka sasa hakuna kinachoendelea.

“Wasiwasi wetu ni kwamba Polisi hawana utayari wa kuchunguza tukio hili ndio sababu wamekuwa kimya mpaka sasa na hakuna kinachoendelea,” alisema wakili huyo.

Alipoulizwa kuhusu mawasiliano na Ofisi ya Bunge ambayo Lissu alipata kudai kuwa linapaswa kugharamia matibabu yake alisema mpaka sasa wana zaidi ya mwezi mmoja na siku 15 bila kuwa na mawasiliano ofisi ya Bunge.

“Familia ilipokea barua ya Bunge Februari mosi, mwaka huu ikitutaarifu kupokea barua yetu ya Januari iliyowataarifu kuhamishwa kwa Lissu kwenda Ubelgiji kutoka Hospitali ya Nairobi alikolazwa tangu apigwe risasi,” alisema Wakili Mughwai.

Alisema barua hiyo iliwataarifu kwamba Ofisi ya Bunge iliwasiliana na Wizara ya Afya  ambayo ilituma madaktari watatu kwenda Nairobi kwa ajili ya kumuona lakini walikuta amekwishapelekwa Ubelgiji.

“Kwenye barua hiyo, Bunge limetushukuru wanafamilia kwa ushirikiano wetu wa dhati wa kuwajulisha kuhusu Lissu alivyoondoka Nairobi kwenda Ubelgij,” alisema Wakili Mughwai.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi Septemba 7, mwaka jana na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye alihamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya mazoezi ya viungo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles