30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Afrika yakoleza joto kujitoa ICC

uhuru-kenyatta-4
Uhuru Kenyatta

 

Markus Mpangala na Mtandao,

NCHI 34 za Bara la Afrika ni miongoni mwa wanachama 122 wa mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliyoanza kufanya kazi Julai 1, 2002. Licha ya ICC kuwa na wanachama wengi kutoka Bara la Afrika, hali imekuwa tofauti kwa muda wa miaka mitatu sasa, uhusiano wa mahakama hiyo na wanachama hao si mzuri. Mwamko wa mataifa ya Afrika kupambana na ICC umetokana na madai kuwa viongozi wengi wanaoshtakiwa wanatoka Bara la Afrika tofauti na kwingineko.

Ikumbukwe kuwa kati ya majaji 17 wa Mahakama ya ICC, watano wanatoka Bara la Afrika pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu, Fatou Bensouda ambaye ni raia wa Gambia. “Tumefikia uamuzi ya kuwa mahakama hii ambayo kwa ujumla Bara la Afrika liliunga mkono kuanzishwa kwake, inaonekana kutotenda haki kwa watu wote,” hiyo ilikuwa kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliyoitoa Novemba 19, 2015.

Waziri huyo alikuwa akizungumza kwa niaba ya umoja huo wa Afrika katika mkutano mkuu unaohusisha mataifa yapatayo 123 yaliyotia saini uanzishwaji wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa ya ICC yenye makao yake mjini The Heague nchini Uholanzi.

Viongozi wa Afrika wanasema Mahakama ya ICC imekuwa ikizilenga zaidi nchi za Afrika na hivyo haitendi haki. Kauli hiyo inapingwa na ICC kwa madai inafuatilia kila hatua ya mchafuko kwenye nchi mbalimbali.

BURUNDI

Taifa hili limekuwa taifa la kwanza kujiondoa rasmi katika mkataba wa Roma unaosimamia Mahakama ya Kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita (ICC). Hatua hiyo imejiri baada ya Rais wa taifa hilo, Pierre Nkurunziza, kutia saini sheria iliyopitishwa na Bunge pamoja na Seneti ya kuiondoa Burundi katika mkataba huo.

Bunge hilo liliidhinisha mpango wa Baraza la Mawaziri kukata uhusiano na mahakama hiyo. Kwa upande wa Mahakama ya ICC, imebainisha kuwa uamuzi wa Burundi wa kujiondoa ni ‘pigo’ katika vita dhidi ya watu wasioheshimu sheria. Mwendesha mashtaka wa ICC alinukuliwa akisema kuwa itachunguza kile kilichotokea Burundi wakati wa maandamano dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza.

Aidha, aliyekuwa waziri wa haki nchini Senegal, Sidiki Kaba, ambaye anaongoza Bodi ya ICC, ametoa wito kwa Burundi kuzungumzia wasiwasi wake badala ya kujiondoa katika mahakama hiyo.

AFRIKA KUSINI

Limekuwa taifa la pili kuanzisha mchakato wa kujiondoa kutoka uanachama wa Mahakama ya ICC. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Serikali ya Afrika Kusini, imesema imechukua uamuzi wa kuanzisha mchakato huo kufuatia shinikizo ililokumbana nalo mwaka jana kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita za kuitaka imkamate Rais wa Sudan, Omar al Bashir, wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika mjini Johannesburg.

Sakata hilo lilitokea Septemba mwaka jana, ambapo Mahakama Kuu ya Afrika Kusini iliinyima Serikali ya nchi hiyo ruhusa ya kukata rufaa uamuzi ulioishutumu kwa kukosa kumkamata Omar al Bashir aliposhiriki mkutano huo Juni 2015.

Serikali ya Afrika Kusini ilijaribu kukata rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu ikisema Al Bashir alikuwa na kinga ya urais kwa sababu yeye ni kiongozi wa taifa, lakini Jaji Hans Fabricius, alipinga suala hilo na kusema rufaa hiyo haiwezi kufanikisha chochote.

“Afrika Kusini ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita na mkataba huo unabatilisha sheria zote ambazo huenda zingempa kinga Bashir asikamatwe na kushtakiwa,” amesema Jaji Hans Fabricius.

Ikumbukwe mwaka jana Chama tawala cha Afrika Kusini, ANC kilitamka hadharani kuwa Mahakama ya ICC imepoteza mwelekeo na haiwezi tena kutimiza wajibu wake.

Kiongozi wa Tume ya Mahusiano ya Kimataifa ndani ya chama cha ANC, Obed Bapela, alisema: “Baraza la kitaifa la Afrika Kusini limeamua kuwa Afrika Kusini inapaswa kujitoa katika Mahakama ya ICC lakini hilo litafanyika tu baada ya sisi kufuata hatua kadhaa.”

GAMBIA

Ni taifa jingine la Afrika ambalo limetangaza kujitoa uanachama kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), ikiituhumu mahakama hiyo kwa kuwalenga viongozi wa Afrika peke yake.

Uamuzi huu wa taifa masikini kwenye ukanda wa Afrika Magharibi, inafuatia ule wa Serikali ya Burundi na Afrika Kusini ambazo zilitangaza kujiondoa kwenye mahakama hiyo.

Uamuzi huo umeelezwa na Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fato Bensouda, kuwa ni pigo kwa mahakama hiyo pamoja na ofisi ya mwendesha mashtaka huyo ambaye raia wa Gambia ambaye aliwahi kuwa waziri wa sheria wa nchi hiyo.

Waziri wa Habari wa Gambia, Sheriff Bojang, ndiye aliyetoa tangazo hilo kupitia televisheni ya taifa, ambapo amesema Mahakama hiyo imekuwa ikiwaacha viongozi kutoka nchi za Magharibi. Kwenye taarifa yake alitolea mfano kesi dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, ambaye mahakama hiyo iliachana na mpango wa kumfungulia mashtaka kutokana na kuhusika kwake kwenye vita ya Irak.

“Kuna nchi nyingi sana za Magharibi, angalau 30, ambazo viongozi wake wametekeleza makosa ya uhalifu wa kivita dhidi ya mataifa huru na watu wake toka mahakama hiyo ilipoundwa, lakini hakuna kiongozi hata mmoja ambaye amepelekwa mbele ya mahakama hiyo,” alisema Waziri Bojang.

Tangu kuanzishwa kwa Mahakama ya ICC mwaka 2002, imekuwa ikituhumiwa kwa upendeleo dhidi ya viongozi wa nchi za Magharibi na badala yake inawalenga viongozi wa Afrika peke yake. Nchi ya Gambia, mara kadhaa imejaribu kutumia Mahakama hiyo kuushtaki Umoja wa Ulaya kwa kuhusika na vifo vya mamia ya raia wake waliokufa kwenye bahari ya Mediterranean bila mafanikio.

SUDAN

Taifa hili linafahamika kuwa si mwanachama wa ICC, lakini Rais wake Omar al Bashir, amedaiwa kutolewa hati ya kukamatwa kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama. Sudan ni kama Marekani ambayo si mwanachama wa ICC na Serikali ya Rais Obama ilipitisha sheria ya kutoruhusu raia wake wanashtakiwa kwenye Mahakama hiyo.

Al Bashir amekuwa akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na makosa ya uhalifu katika Jimbo la Darfur. Kiongozi huyo aliyechukua madaraka baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 amekuwa akisakwa na Mahakama ya ICC kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na makosa ya uhalifu wa kivita katika Jimbo la Darfur, madai ambayo Bashiri amekanusha. Mwaka 2009 Mahakama ya ICC ilitoa hati ya kumkamata kiongozi huyo.

SUDAN KUSINI

Tangu kuundwa kwa taifa hili mwaka 2009, limeshindwa kujiunga na kuwa mwanachama wa ICC. Rais Salva Kiir, haonekani kuwa na haraka ya kujiunga na Mahakama hiyo, huku akikabiliwa na changamoto mbalimbali ndani ya taifa lake kutokana na machafuko yanayozuka mara kwa mara.

KENYA ITAFUATA?

Septemba, 2013 baada ya mjadala mkali wa Bunge la Kenya, lilipitisha muswada wa kuitaka nchi hiyo kujiondoa katika mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya ICC. Hatua hiyo ilikuja wakati Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto, walipokuwa wakikabiliwa na kesi zao kabla ya kufutwa, zilizotokana na machafuko ya kisiasa kati ya mwaka 2007 na 2008.

Wakati wa kuwasilishwa muswada huo baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Kenya, waliondoka kwa hasira bungeni wakati mjadala huo ulipokuwa unaendelea. Wabunge hao waliondoka baada ya kusema kuwa kamwe hawataungana na upande wa Serikali kuunga mkono hoja hii ya kujiondoa kutoka katika Mahakama ya ICC.

Wengi waliounga mkono hoja hiyo walikuwa wabunge wa muungano tawala wa Jubilee unaoongozwa na vigogo Rais Uhuru Kenyata na naibu wake, William Ruto. Naibu Kiongozi wa upinzani bungeni, Jakoyo Midiwo, alisema kuwa wabunge wa upande wa Serikali wanaotetea hoja hiyo ya kujiondoa ICC  watakuja kujuta.

MSIMAMO WA AU

Mapema mwaka jana, marais wa Umoja wa Afrika (AU), walipitisha pendekezo kutafuta njia ambayo bara la Afrika lingeweza kujiondoa katika mahakama hiyo kwa pamoja. Kumekuwa na malalamiko kwamba mahakama hiyo inalenga masuala ya Afrika pekee. Kesi zote zinazoangaziwa na mahakama hiyo zinatoka Afrika. Kutokana na msimamo huo, viongozi kadhaa wa Afrika wamekataa kumkamata Omar al Bashir na kumfikisha mikononi mwa ICC. Viongozi hao ni Rais Jacob Zuma (Afrika Kusini), Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda), marehemu Bingu wa Mutharika (Malawi).

TUHUMA NA UTETEZI WA ICC

Licha ya kurundikiwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kesi zinazowalenga viongozi wa Afrika pamoja na Rais wa Mahakama hiyo kudaiwa kupokea rushwa, ICC imeeleza nia yake ya kuendesha kesi kwa haki na kwamba suala la Burundi litakuwa miongoni mwa mambo yanayochunguzwa ili kufungua shauri.

Tuhuma nyingine ni ile ya Rais wa ICC, Silvia Alejandra Fernandez de Gurmendi ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huru wa madai ya ufisadi wa kifedha dhidi yake katika kesi dhidi ya Rais wa Sudan, Omar al-Bashir.

Kwa mujibu wa gazeti la London Evening Post la Uingereza toleo la Julai 3, mwaka huu liliripoti kuwa, Silvia Alejandra Fernandez de Gurmendi, anatuhumiwa kupokea mamilioni ya dola za Marekani ili kuwahonga mashahidi bandia katika kesi dhidi ya Rais wa Sudan.

Aidha, lilieleza kuwa, Jaji Fernandez de Gurmendi, alipokea jumla ya dola milioni 17 za Marekani kati ya mwaka 2004 na 2015 kutoka mashirika kadhaa yakiwemo Barting Holding Ltd, Atlantic Corporation, Genesis International Holdings na Napex International wakati ICC ilikuwa inafanya uchunguzi dhidi ya Bashir. Gazeti hilo limeandika kuwa, fedha hizo zilitumwa katika akaunti za makundi ya waasi kama vile Sudan Liberation Movement ambayo awali ilifahamika kama Darfur Liberation Front 2002.

Mashinikizo ya kujiuzulu Rais wa ICC yamejiri katika hali ambayo Rwanda hivi karibuni ilitupilia mbali wito wa kumkamata Rais Omar al-Bashir na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC alipozuru nchi hiyo kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika mjini Kigali.

Akizungumzia sakata hilo la kumkamata Al Bashir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louis Mushikiwabo, alisema nchi hiyo mbali na kuwa si mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni ICC, lakini ilikataa kumkamata Rais wa Sudan kwa madai kuwa mahakama hiyo ‘imegubikwa na siasa’ na kwamba imekuwa ikitumika kuwaandama viongozi wa bara la Afrika tu.

Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, ameutetea utendaji wa Mahakama hiyo na kusema bado mahakama hiyo ina wajibu muhimu katika kuzingatia sheria na haki. Aidha, shutuma dhidi ya Rais wa Mahakama hiyo zimepuuzwa hadi sasa kwakuwa si ICC yenyewe wala Jaji Fernandez de Gurmendi aliyejitokeza kukanusha kwa muda wa miezi mitatu sasa.

Naye mwendesha mashtaka wa zamani wa Mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo, alitetea mwenendo wa ICC na kuilaumu Burundi kutenda jinai. Akizungumza na Shirika la Habari la Al Jazeera, alisema: “Burundi inajitoa ICC kwa madhumuni ya kuendeleza uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu. Afrika Kusini nayo inaungana na Burundi kubariki vitendo viovu vya kuwaacha huru viongozi watende uhalifu na mauaji ya Kimbari pamoja na watu wasio na hatia.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles