MSANII anayetamba kwa sasa duniani na wimbo wa ‘Hello’, Adele Adkins, amemshangaa mgombea urais nchini Marekani kupitia tiketi ya chama cha Republic, Donald Trump, kwa kutumia wimbo wake katika kampeni.
Mgombea huyo amekuwa akiutumia wimbo wa Adele wa ‘Rolling in the Deep’, bila idhini ya msanii huyo wimbo huo aliuachia mwaka 2011.
“Sijatoa idhini ya wimbo wangu kutumika kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini Marekani, ila nashangaa kuona Trump akiutumia wimbo wangu wa zamani katika kampeni zake bila makubaliano yoyote,” aliandika Adele kwenye mtandao wake wa Twitter.
Hata hivyo, mgombea mwingine, Mike Huckabee, anautumia wimbo mpya wa msanii huyo unaojizolea umaarufu duniani wa ‘Hello’ katika video moja ya kampeni yake iliyochapishwa kwenye mtandao wa Youtube.
Hata hivyo, Adele hakubainisha kama atachukua hatua za kinidhamu dhidi ya wote wanaocheza nyimbo zake bila idhini yake.