SAM BAHARI – SHINYANGA
MKAZI wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, Shaibu Jabuka (36) anadaiwa kujeruhiwa kwa kukatwa korodani kwa wembe na mke wake aliyefahamika kwa jina moja la Mwajuma, baada ya kumnyima Sh 10,000 ya matumizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Deborah Magiligimba, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 6 mwaka huu, saa 7.00 usiku huko Ngokolo nyumbani kwa wanandoa hao.
Kamanda Magiligimba alisema Chanzo cha tukio hilo ni Mwajuma kunyimwa na mumewe Sh 10,000 ya matumizi.
Alisema siku ya tukio majira ya saa saba usiku wakiwa wamelala nyumbani kwao, Jabuka alianza kuomba tendo la ndoa kwa mkewe ambaye naye alianza kuomba apewe fedha za matumizi kwanza ndipo washirika tendo hilo.
Kamanda Magiligimba alisema katika mabishano hayo mwanaume huyo alianza kutumia nguvu kwa kumgeuza mkewe akihitaji kufanya tendo hilo.
Inadaiwa baada ya mwanaume kufanikiwa kufanya tendo la ndoa na mkewe, mwanaume alilala na ndipo mke wake alipoamka na kumkata mumewe korodani ya kulia kwa kutumia wembe.
Alisema Jabuka alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kupatiwa matibabu na kuruhusiwa na kurejea nyumbani kwake.
Alisema Mwajuma alitoroka mara baada ya tukio na kukimbilia kusikojulikana na kwamba juhudi za kumtafuta zinaendelea na atakapokamatwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kamanda Magiligimba alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hususani wanandoa au wenye mahusiano ya kimapenzi, kuacha oja kujichukulia sheria mkononi bali wafikishe migogo yao kwa wazee wenye busara, Ofisi za Ustawi wa Jamii na Dawati la Jinsia na Watoto zilizoko katika vituo vya polisi.