26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

ACT YAMFICHA ZITTO KABWE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


CHAMA cha ACT- Wazalendo, kimemficha kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, baada ya kuenea kwa taarifa za kusakwa kwa mbunge huyo.

Katika kile kinachoonekana kufichwa kwa mbunge huyo ambaye tangu juzi hapatikani kwa mawasiliano ya simu yake, jana katibu wake, Deodatus Wiston, alitoa taarifa ya kuahirishwa kwa mkutano wa Zitto kutokana na hofu ya kiusalama kwa mbunge huyo.

Zitto tangu alipoibua hoja kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu zilipo Sh trilioni 1.5, ambapo wiki iliyopita CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi  wa chama hicho, Humphrey Polepole, alivitaka vyombo vya dola kumkamata mbunge huyo kwa kuwa amepotosha kuhusu wizi huo wa fedha.

Pamoja na hali hiyo pia Serikali ililazimika kutoa kauli bungeni na kusema hakuna wizi wa kiasi hicho cha fedha.

Taarifa iliyotolewa jana na katibu wa mbunge huyo, ilieleza kuahirishwa kwa mkutano wa Zitto hadi itakapotangazwa tena kutokana na sababu za kiusalama.

“Mkutano wa ndani wa Mbunge umeahirishwa mpaka hapo tutakapowatangazia. Sababu kubwa ni masuala ya usalama wa mbunge wetu na hivyo tumeona tuahirishe na kujipanga upya,” alisema Wiston katika taarifa yake.

MTANZANIA ilipomtafuta Ofisa Habari wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis kuhusu taarifa ya kusakwa kwa mbunge huyo, alisema hawajapata taarifa za kuitwa polisi kwa mbunge huyo ila kama wanamuhitaji yupo tayari kwenda.

“Ni kweli mkutano umeahirishwa kutokana na sababu za kiusalama, hili la kutafutwa na polisi bado sijalisikia lakini kama kweli Polisi wanamsaka kiongozi wetu wa chama wasitumie nguvu kubwa wampigie simu naye atakwenda kuitikia wito,” alisema Zitto.

Hata hivyo jana mwanahabari mkongwe nchini, ambaye anaishi uhamishoni nchini Finland, Ansbert Ngurumo,  aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter, kuna haja ya kushughulikiwa watu wanaokosoa Serikali akiwamo Zitto Kabwe, kutokana na kufichua kashfa ya Sh trilioni 1.5.

Hata hivyo Jeshi la Polisi lilipoulizwa kuhusiana na madai hayo, kupitia kwa Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema wao hawafanyi kazi kupitia taarifa za kwenye mitandao ya kijamii.

“Taarifa za kwenye mitandao, polisi inahusika namna gani hapo?…muulizeni aliyetoa. Taarifa zozote lazima ziwe na chanzo, Jeshi la Polisi limegawanyika katika mikoa, vikosi na makao makuu. Hawezi kusakwa tu na polisi…ni kamanda wa mkoa gani na anamtaka Zitto kwa kosa gani?,” alihoji Mwakalukwa.

Katika siku za hivi karibuni Zitto na chama chake walifanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kudai kuwa kuna upotevu wa Sh trilioni 1.5.

Hata hivyo kumekuwa na kila dalili zinazoonyesha kwamba, ubishani kuhusu zilipo Sh trilioni 1.5 bado haujafika mwisho, licha ya Rais Dk. John Magufuli na Serikali yake kuzitolea ufafanuzi mwishoni mwa wiki.

Pamoja na hali hiyo jana Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aeshi Hilaly alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa tayari wamepanga kumwita CAG, Profesa Mussa Assad, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James pamoja na timu yake muda wowote kuanzia sasa, ili watoe majibu.

“Solution (suluhisho) ipo kwenye kamati yetu, sisi ndio tuna majibu yote, tutamwita CAG, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na timu yake watoe majibu,” alisema Aeshi.

Alipoulizwa hatua ambazo watachukua endapo majibu ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango au yale ya CAG hayatawaridhisha, Aeshi alisema tutamwagiza CAG kwenda kufanya ukaguzi upya.

“Haya mambo yanahitaji hoja na vielelezo vya kuthibitisha, sasa kama hatutaridhika tutamwagiza kufanya verification (kuthibitisha) au ukaguzi na baada ya hapo atarudi kwenye kamati ya PAC kutoa maelezo,” alisema Aeshi.

Kauli hiyo ya PAC imekuja wakati ambao tayari Rais Dk. John Magufuli, amelitolea ufafanuzi suala hilo, tena kwa kumwuliza CAG kama fedha hizo zimepotea, naye akijibu hazijapotea.

Kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ililazimika kulifafanua suala hilo bungeni mwishoni mwa wiki, akikanusha kupotea kwa fedha hizo.

Akifafanua ilipo hiyo Sh trilioni 1.5, Dk. Kijaji alisema Sh bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh bilioni 689.3 mapato tarajiwa na Sh bilioni 203.9 ni mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Zanzibar.

“Kuanzia mwaka 2016/2017, TRA ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual, hivyo kati ya mapato haya ya Sh trilioni 25.3, yalikuwepo pia mapato tarajiwa kama mapato ya kodi ya Sh bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar ya Sh bilioni 203.92,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema katika uandishi wa taarifa yake,  CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti, ambapo hadi Juni 2017, mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa Sh trilioni 23.79.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva, matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika, hivyo basi baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh trilioni 24.4,” alisema Kijaji.

Kauli hiyo ya Dk. Kijaji inarandana na ile iliyotolewa mwanzo kabisa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Pamoja na ufafanuzi huo wote, Zitto yeye anasisitiza kwamba, fedha hizo Sh trilioni 1.5 kati ya Sh trilioni 25.3 za mapato yaliyokusanywa katika uchambuzi wake wa ripoti hiyo ya CAG umeonyesha hazina nyaraka zinazothibitisha katika matumizi ya Serikali.

Tayari amekwishatamka kwamba, kama Serikali ina uhakika hoja hiyo haipo katika ripoti hiyo ya CAG, basi impeleke mahakamani na ataishinda kwa sababu sasa anazo nyaraka za kuthibitisha zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles