23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

FATMA KARUME: HAKUNA WA KUIDHIBITI TLS

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kumtaka Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, kukidhibiti Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Rais wa chama hicho, Fatma Karume ameibuka na kusema kuwa hakuna wa kukidhibuti chama hicho.

Fatma ambaye alishinda urais wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika Aprili 14, mwaka huu akirithi nafasi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Tundu Lissu, alisema TLS haiendeshwi na chombo chochote pamoja na kwamba iko chini ya Mahakama.

Ijumaa iliyopita wakati akiwaapisha, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na majaji kumi wa Mahakama Kuu, Rais Magufuli alimhoji Profesa Juma endapo TLS ni mali ya umma.

Kutokana na hilo, Profesa Juma alimjibu kuwa chama hicho cha mawakili ni mali ya umma, ndipo mkuu huyo wa nchi akamtaka kuidhibiti TLS.

“Kama ni mali ya umma, sasa isiwe mali ya mtu binafsi…kwa hiyo AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) yupo na  wewe Jaji Mkuu upo nyinyi ndiyo mnaishikilia hiyo mali ya umma, sasa mali ya umma isije ikakosa control ikawa mali binafsi.

“Nchi hii tunataka nidhamu na mimi nataka nikuhakikishie jaji kuwa tutasimamia nidhamu, katika yale yaliyokuwa yanazunguka fedha za bajeti ya mahakama imeshushwa chini.

“Fedha za maendeleo zimeshushwa chini kwa hiyo kuna wasemaji wengi wa wizara na nimemsikia mmoja anasema mishahara yenu ni midogo, sijui anawaombea mishahara?

“Mnisaidie tu kwa hawa mnawaotuma ambao ni wasemaji wenu kwa sababu wanawachonganisha na mimi, nashindwa kutofautisha kama amejituma au mmemtuma,”alisema Rais Magufuli.

KAULI YA FATMA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Fatma alisema TLS inajiendesha yenyewe na kwamba wanachama wake ambao ni wanasheria wanalipa ada ya kila mwaka, fedha ambayo inawalipa mishahara wafanyakazi 40 bila msaada kutoka chombo chochote.

“TLS inaendeshwa na wanachama kwa fedha zao wenyewe, kila mwaka wanachama wanatoa ada na tunawalipa wafanyakazi 40 mishahara yao bila msaada kutoka kokote, tunawahudumia wananchi kwa fedha zetu wenyewe.

“Mahakama ni mhimili ambao uko huru na Serikali ni mhimili mwingine ambao nao uko huru. Kama wanasheria sisi tuko chini ya Mahakama.

“Hivyo hakuna mtu wa kuidhibiti TLS kwa sababu hakuna binadamu anayeweza kumdhibiti binadamu mwenzake kwa mujibu wa katiba yetu kila binadamu ni huru, lakini unapovunja katiba na sheria za nchi hapo hauko huru.

“TLS tuko huru kabisa kwa sababu hakuna sheria ambayo tunaivunja. TLS haiendeshwi na chombo chochote,”alisema Fatma.

Naye wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole, aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa TLS si mali ya umma kwa sababu hawapewi ruzuku na Serikali.

“Wafanyakazi wa TLS hawalipwi wala kuchaguliwa na Serikali, CAG (Mdhibiti wa Hesabu wa za Serikali) hakagui hesabu za TLS, viongozi hatuchaguliwi na Serikali, hakuna hata kifungu kimoja cha sheria kinasema Jaji Mkuu au Mwanasheria Mkuu ndiyo mabosi wetu.

“Sasa kama tukiwa ni sehemu ya Serikali tutateteaje kesi dhidi ya Serikali? Sisi ni taasisi huru tangu mwaka 1954, tumeanza kabla Tanzania hata mkoloni hakuwahi kutuingilia,”aliandika wakili huyo.

Wiki iliyopita baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Rais wa TLS, Fatma Karume, alipinga kupunguzwa kwa bajeti ya idara ya mahakama jambo ambalo alisema hawaliungi mkono.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles