Na Patricia Kimelemeta – dar es salaam
SIKU moja baada ya kuwapo taarifa za Rais Dk. John Magufuli kutaka kuzungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari leo, Chama cha ACT-Wazalendo kimemtaka kiongozi huyo kusikiliza ombi la kusogeza mbele Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 hadi Februari mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Addo Shaibu, alisema chama hicho kimeupitia muswada huo na kuona bado kuna haja wadau wa habari kukaa chini na kuanza kuupitia kipengele kimoja baada ya kingine.
Alisema kuharakishwa kupelekwa bungeni kusomwa kwa mara ya pili na kuupitisha haraka, kunaonyesha wazi kuna mambo yamejificha, ambayo Serikali inataka kuyaficha ili wanahabari washindwe kutimiza majukumu yao.
“ACT-Wazalendo imeshangazwa na kitendo cha Serikali kuharakisha kuupeleka bungeni Muswada wa Habari wakati kuna upungufu mwingi katika baadhi ya vipengele, jambo ambalo linahitaji muda zaidi ili waweze kuupitia na kutoa maoni, kwa sababu kesho (leo) Rais Magufuli ametangaza kuzungumza na wahariri na waandishi wa habari, anaweza kutumia muda huo kusikiliza malalamiko yao,” alisema Shaibu.
Alisema kinachoonekana sasa hivi muswada huu umeletwa kuzika uhuru wa habari na utoaji wa mawazo au ushauri kwa Serikali ya awamu ya tano, jambo ambalo linaweza kuficha maovu ya Serikali.