25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kangi, Kibajaji wazidi kuwabana mawaziri

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola

Na Bakari Kimwanga, DODOMA

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamezidi kuwabana mawaziri na kusema huenda hawamshauri vizuri Rais Dk. John Magufuli kuhusu hali ya uchumi.

Akizungumza bungeni Dodoma jana, wakati akichangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/18, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, aliwaonya mawaziri ambao wamekuwa wakimpotosha Rais Magufuli kuwa fedha zimepotea kutokana na baadhi ya watu kuficha majumbani kwenye magodoro,  wakati hiyo si sababu.

“Nyinyi mawaziri ni abiria na mmekaa siti za mbele kwenye gari analoendesha Rais Magufuli, msimkimbize… baadhi yenu msimpotoshe. Yeye si mchumi, mtamletea matatizo siku zijazo, fedha zimepotea si  kwa sababu zimefichwa kwenye magodoro ila zimepotea kwa sababu zimewekwa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), zitoeni hizo ziende kwenye benki za kawaida,” alisema.

Alisema hivi sasa Bunge limepoteza mwelekeo, baada ya kulialia kila siku kumlaumu rais kwa sababu amebana wakwepakodi.

“Rais aliliomba Bunge hili limsaidie kutumbua majipu, tumsaidie mipango ya Serikali iweze kutekelezeka ili kujenga nchi yetu, najua ana nia njema, lakini “hapa kazi tu” inawafanya wafanyabiashara waliozoea kukwepa kodi wamebanwa, sasa wanalia biashara imekufa.

“Watumishi waliozoea posho za hapa na pale, kusafiri wamebanwa, wabunge tuliozoea kula andazi la inchi 18, sasa tunakula la sentimeta mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, tunalialia, tumeshikwa pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge eti hawana fedha,” alisema Lugola.

Pamoja na hali hiyo, alitupa kombora kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akidai kuwa amepewa gari na Serikali na mafuta, huku akipulizwa na kiyoyozi kwa saa 24 hivyo anapaswa kuwa mkweli.

“Unasema Serikali imefilisika, unawachonganisha wananchi na rais wao, unawatumia vibaya wananchi, (Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter) Msigwa kama mchungaji tumia taaluma yako kuwashauri wenzako wawe kwenye safari hii… Rais Magufuli anatupeleka Kaanan kuishi maisha mazuri, ametupandisha basi kutupeleka nchi ya ahadi.

“Nashauri anapoendesha gari ajue kuna matuta akiendesha vibaya Watanzania atatuangusha, kuna zebra na wanafunzi wanavuka, akiona spidi ikiwa 50  apunguze mwendo… na nyinyi mawaziri mmekaa siti za mbele za gari la rais msimpotoshe,” alisema.

LUSINDE

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema uchumi unapokua lazima uonyeshe maisha ya wananchi wa vijijini na si utoaji wa pointi kwenye makaratasi.

“Upinzani msizunguke kusema Serikali imefilisika, semeni ukweli Mbowe umefilisika, umeshindwa kulipa madeni, Serikali haijafilisika inalipa mishahara, inalipa madeni yake,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles