22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

‘Acheni starehe fanyeni kazi kupunguza utegemezi’

Vijana wakicheza pool. Utafiti uliotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), unaonyesha Watanzania wengi wanatumia muda mwingi kustarehe badala ya kufanya kaziNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

UTAFITI wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wa 2014/15, umeonesha asilimia 71 ya Watanzania walio katika umri wa kufanya kazi wanapenda kula ‘bata’.

Kundi hilo ni la wale wanaoanzia umri wa miaka mitano na zaidi ambapo utafiti huo umeeleza huwa wanafanya shughuli za kustarehe, kulala na kujihudumia wenyewe.

Meneja wa Ajira na Bei wa NBS, Ruth Minja, ni mmoja wa wasimamizi waliohusika katika ukusanyaji wa takwimu za utafiti huo zilizokusanywa kote nchini.

Anasema watu wenye umri wa kufanya kazi katika mwaka 2014/15 walikuwa milioni 25.7 kati yao wanaume ni milioni 12.4 na wanawake ni milioni 13.4.

Anasema kati ya hao nguvu kazi ya Taifa ilikuwa ni milioni 22.3 wanaume walikuwa milioni 11.0 na wanawake walikuwa milioni 11.2.

Anasema katika kundi hilo la nguvu kazi watu milioni 20 walikuwa kwenye ajira, wanaume wakiwa milioni 10.1 na wanawake ni milioni 9.8. Watu milioni 2.3 hawakuwa na ajira, ambapo wanaume walikuwa 900,000 na wanawake milioni 1.4.

“Kati ya wale waliokuwa na umri wa miaka 15 na kuendelea ambao walikuwa nje ya nguvu kazi ya Taifa walikuwa milioni 3.4, wanaume wakiwa milioni 2.3 na wanawake 2.1,” anasema Minja.

Anasema utafiti huo ulifanywa kwa kuzingatia viashiria 18 vinavyoshauriwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambavyo nchi yoyote ikivitumia inapata picha ya haraka ya hali ya soko la ajira nchi mwake.

“Kiashiria cha kwanza ni kiwango cha ushiriki wa nguvu kazi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi… hiki ni kipimo cha uwiano wa nguvu kazi na watu wenye uwezo wa kuanya kazi nchini,” anasema.

Anasema kiwango cha ushiriki wa nguvu kazi kuanzia miaka 15 kilichopo katika shughuli za uzalishaji wa bidhaa za kiuchumi kimepungua kutoka asilimia 89.6 mwaka 2006/7 hadi kufikia asilimia 86.7 mwaka 2014/15.

Kulingana na Meneja huyo, kiashiria namba mbili ni uwiano kati ya ajira na watu wenye uwezo na umri wa ambapo matokeo yanaonesha kwamba kiwango cha uchumi kuzalisha ajira kwa kuzingatia kiashiria cha uwiano kati ya ajira na watu wenye umri wa kufanya kazi kimepungua kutoka asilimia 79.2 mwaka 2006/7 hadi asilimia 77.8 mwaka 2014/15 huku wanaume wakiwa na kiwango kikubwa zaidi.

Anasema kiashiria cha tatu ni kiwango cha hali ya ajira nchini ambacho kimewekwa katika makundi makubwa manne ambao ni watu walioajiriwa kwa malipo, waliokuwa wamejiajiri wenyewe, wanaofanya kazi ya kifamilia na wakulima.

“Kwa kuzingatia kiashiria hicho utafiti umebaini kwamba kiwango cha wakulima waliokuwa wameajiriwa kwa malipo kimeongezeka kutoka asilimia 10.5 mwaka 2006/7 hadi asilimia 13.8 mwaka 2014/15. Hata hivyo kiwango cha ushiriki katika shughuli hizo kimeshuka kutoka asilimia 75.1 hadi 65.7 katika kipindi hicho,” anasema.

Meneja huyo anasema kushuka kwa kiwango hicho cha ushiriki katika upande wa kilimo, kumeonesha kukua kwa sekta nyingine binafsi.

Anasema kiashiria kingine ni sekta za ajira kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ambapo kiwango cha ajira katika sekta isiyo rasmi kimeongezeka kutoka asilimia 10.1 mwaka 2006/7 hadi kufikia asilimia 21.7 mwaka 2014/15.

“Kiashiria cha tano ni ajira kwa aina ya kazi ambapo kiwango cha watu kujishughulisha na kilimo kimepungua kutoka asilimia 73.1 hadi 66.3 hata hivyo kwa upande wa ajira zisizo rasmi kiwango kimeongezeka zaidi ya mara mbili kutoka asilimia 10.1 hadi 27.3,” anasema.

Anasema kiashiria kingine ni kiwango cha saa za kazi matokeo ya utafiti yanaonesha kumekuwa na ongezeko la saa kwa makundi yote ikiwamo wale wanaofanya kazi kwa malipo, waliojiajiri na wakulima.

“Utafiti umebaini kwamba watu wanaofanya kazi za malipo na za kujiajiri wenyewe wanatumia zaidi ya saa 50 kwa wiki kuliko kada nyingine za ajira. Takwimu hizi zitasaidia kuboresha sera za ajira na nyinginezo ili kuwe na uwiano kati ya saa watu wanazofanya kazi na uzalishaji na malipo yao,” anasema.

Anasema kiashiria cha nane walichokizingatia ni ajira zisizo rasmi katika sekta rasmi na isiyo rasmi kati ya ajira zote nchini matokeo yanaonesha kulikuwa na ongezeko karibu mara mbili ya ajira hizo kutoka asilimia 10.1 hadi asilimia 27.3 katika kipindi hicho.

Anasema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa watu wenye umri wa miaka 15 kimepungua kidogo kutoka asilimia 11.7 hadi 10.3 katika kipindi hicho.

“Kundi la wanawake ndilo linaongoza kwa kukosa kazi huku vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 13.2 hadi 1.7,” anasema.

Anasema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa muda mrefu kimeongezeka kutoka asilimia 17.9 hadi 32.5. Hii inaashiria kuwa watu walitumia muda mrefu kutafuta kazi mwaka 2014 ikilinganishwa na mwaka 2006 huku kundi la wanawake likiwa  na asilimia kubwa.

“Matokeo yanaonesha kiwango cha watu waliofanya kazi chini ya muda wa kazi ambao ni saa 40 kwa wiki lakini bado walikuwa wanahitaji kufanya kazi zaidi walikuwa ni asilimia 7.8 hadi 11.8, takwimu hizi zitasaidia kuboresha sera ili kutumia vizuri rasilimali watu maana hawa walitaka kufanya kazi zaidi,” anasema.

Anasema kiwango cha watu ambao hawakuwa na kazi na wala hawakuwa tayari kutafuta kazi kimeongezeka kutoka asilimia 10.4 hadi 17.2, wanawake wakiwa na kiwango kikubwa zaidi kuliko wanaume.

Anasema matokeo yanaonesha kiwango cha nguvu kazi wasiojua kusoma na kuandika kimepungua kutoka asilimia 25.8 hadi asilimia 20.1.

Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, anasema yamedhihirisha bado ipo changamoto ya kufanyiwa kazi kwani asilimia 71 ya Watanzania hawataki kufanya kazi zaidi ya kujistarehesha na kulala.

“Eneo hili ni la muhimu kulitazama. Hii ni changamoto lazima wananchi tubadili fikra zetu na kujiletea maendeleo bila ya kukaa na kungojea mtu mwingine au serikali ituletee.

“Ingawa kwa upande wa wanawake utaona wao wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za nyumbani bila malipo ambao ukiupima utakuta wanachangia kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi,” anasema.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama, anasema matokeo hayo yataisaidia serikali katika kupanga sera zake za maendeleo.

“Mgawanyo wa ukosefu wa ajira katika maeneo mbalimbali ya nchi unaonesha Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na kiwango kikubwa cha asilimia 21.5 ikifuatiwa na maeneo mengine ya mijini kwa asilimia 9.9 na vijijini 8.4,” anasema Mhagama.

Anasema jitihada za makusudi zinahitajika zaidi ikiwa ni pamoja na upande wa walemavu ambako kiwango cha ukosefu wa ajira kwa wenye umri wa miaka 15 na kuendelea mwaka 2014/15 ni asilimia 12.4 ambacho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha Kitaifa cha asilimia 10.3.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles