27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Calvin Martin: Bila hesabu, sayansi hatuwezi kupata wahandisi

calvin photo 1NA MAREGESI PAUL, (OUT) DAR ES SALAAM

WAKATI nchi yetu ikiwa katika harakati mbalimbali za kupiga hatua kiuchumi na kusababisha wananchi wengi kubaki maskini, wapo baadhi ya Watanzania wana maono kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za kuondokana na umaskini lakini tatizo lililopo ni wananchi wengi kutowajibika.

Calvin Martin, Meneja wa kiwanda cha kutengeneza Bia cha Tanzania Breweries (TBL) kilichopo Dar es Salaam, ni miongoni mwa Watanzania wanaoamini kuwa nchi inazo fursa nyingi za kuondokana na umaskini, kuboresha huduma za kijamii na wananchi kuishi maisha mazuri.

Ana imani kuwa falsafa ya ‘Hapa Kazi tu’ iliyoanzishwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, ikitekelezwa ipasavyo nchi itapiga hatua kubwa kiuchumi kwa kuwa upo ushahidi wa baadhi ya mataifa hususani barani Asia ambayo kwa kupitia falsafa kama hii wameweza kupiga hatua kubwa kiuchumi.

Anasema ana imani kuwa mtu yeyote akifanya kazi kwa bidii na maarifa ni lazima afanikiwe katika jambo lolote na imani hiyo imemsaidia kufanikiwa katika mambo mengi hadi kufikia hatua alipo.

“Siku zote naamini kuwa kufanya kazi kwa bidii na weledi kunaleta mafanikio na huwa nasikitika sana kuona baadhi ya watu hususani vijana ambao wanakaa bila kufanya kazi wakati wana nguvu za kutosha na nguvu kazi inapotea bure badala ya kushiriki katika uzalishaji kwa manufaa yao na manufaa ya taifa,” anasema.

Anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea Watanzania mazingira mazuri ya kufanya kazi ziwe kwa kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe na kuongeza kuwa ajira nyingi ziko katika sekta ya kilimo, ufugaji, viwanda na kwenye ufundi wa aina mbalimbali.
Anasema alipata elimu ya juu katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), ambako alisomea shahada ya kwanza ya Sayansi na alikuwa miongoni mwa wahitimu waliofanya vizuri mwaka 1993.

Baada ya kumaliza masomo ya shahada ya kwanza, alijiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili chuoni hapo akijikita zaidi katika Sayansi ya Viwanda na Utawala ambako alihitimu mwaka 1997.

Ajira yake ya kwanza ilikuwa katika Kampuni ya East Africa Breweries ambako alikuwa kwenye kitengo cha uzalishaji.

Anasema kwa muda mfupi aliweza kuielewa fani ya uzalishaji bia kwa vitendo na nadharia, kuhitimu Stashahada ya Utengenezaji bia (Diploma in Brewing) ya Uingereza na baada ya kufanya kazi na kampuni hiyo kwa miaka mitatu na nusu aliamua kujiunga katika kampuni ya TBL Group.
Akiwa na kampuni hii ameweza kushika nyadhifa mbalimbali hadi kufikia nafasi aliyo nayo hivi saa ya kusimamia kiwanda cha TBL cha Dar es salaam.

Moja ya kazi kubwa anazojivunia ndani ya kampuni hiyo ni kusimamia ujenzi na uanzishwaji wa kiwanda cha Mbeya.

“Kazi ya kuanzisha kiwanda hiki ilikuwa moja ya changamoto ya kikazi kwangu, lakini kutokana na ujuzi na uzoefu kwa kushirikiana na wenzangu tulifanikiwa na najivunia kuona kiwanda hiki ni moja ya viwanda vya kampuni vinavyofanya vizuri kikiwa chini ya uongozi na wafanyakazi Watanzania,” anasema.

Mbali na kupata elimu za vyuoni akiwa mwajiriwa wa TBL, tayari Calvin amehudhuria kozi mbalimbali ndani ya kampuni ndani na nje ya nchi ambazo zimezidi kumpatia maarifa ya kitaalamu, kiufundi, utawala, uendeshaji na usimamiaji wa viwanda kwa ufanisi.

“TBL kuna mafunzo ya aina nyingi na kuna mitambo ya kisasa na mara nyingi tumekuwa tukipata mafunzo ya aina mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi mfano ‘SABMiller Manufacturing Way’ ambayo tunaitumia na imeonyesha mafanikio makubwa,” anasema.

Pia anasema kuna mafunzo ya utawala na mifumo mbalimbali inayowawezesha mameneja wa viwanda na wakuu wa vitengo kuendesha shughuli zao vizuri wakiwa wanajua jinsi ya kutoa vipaumbele kwenye mambo mbalimbali na mpangilio mzuri wa ratiba za kazi.

Calvin aliongeza kusema kuwa anaweza kufanya kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wafanyakazi wenzake.

“TBL ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu wenye uwezo mkubwa katika fani zao, hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya, wanaojituma bila kuhitaji usimamizi mkubwa,” anasema.

Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela kama kawaida.

Anasema anajivunia kufanya kazi na kampuni kubwa kama TBL Group ambayo imemuwezesha kujifunza mambo mengi ikiwemo kupata mafanikio mbalimbali katika maisha yake mojawapo ikiwa ni kuihudumia familia yake vizuri.

Anatoa wito kwa vijana kutokimbia masomo ya hesabu na sayansi wanapokuwa mashuleni bali wajitahidi kwani katika dunia hii ya sayansi na teknolojia bila wataalamu itakuwa vigumu kwa taifa kupiga hatua za maendeleo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles