26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Acheni roho mbaya, pandisheni watumishi madaraja-Kikwete

Na Gustafu Haule, Pwani

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi waliopo katika Halmashauri mbalimbali nchini kuacha roho mbaya ya kuwawekea watumishi wenzao vikwazo vya kutowapandisha madaraja.

Kikwete ametoa kauli hiyo Julai 11, wakati akizumgumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha vijijini mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuwatembelea watumishi kwa ajili ya kusikiliza kero zao.

Akiwa katika mkutano na watumishi hao Kikwete amepokea kero mbalimbali za watumishi wa halmashauri hiyo ikiwemo kutopandishwa madaraja kwa wakati, kutolipwa fedha za likizo, malimbikizo ya mishahara na hata stahiki nyingine.

Aidha, baada ya kupokea kero hizo Kikwete, amesema kero nyingi zilizopo katika Halmashauri hiyo zinapaswa kutatuliwa na halmashauri husika huku akisema shida kubwa inatoka kwa maafisa utumishi wanaoshindwa kuwajibika katika maeneo.

“Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi wa halmashauri wanashindwa kufanyakazi kwa sababu ya maafisa utumishi kushindwa kuwatatulia kero zao, jambo hli ni kinyume na utaratibu,” amesema Kikwete.

Ameongeza wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mwaka 2021 alikuta kwa miaka Sita watu hawajapandishwa madaraja lakini alipoingia alipandisha madaraja watumishi 70,000.

Amesema rais ameonyesha nia kwamba anataka kulipa madeni ya watumishi pamoja na kuwapa stahiki zao ikiwemo kupandishwa madaraja, vyeo, kulipa mishahara, fedha za likizo na masuala mengine halafu watu wachache wamkwamishe.

Amewataka maafisa utumishi kubadilika na kuacha kufanyakazi kwa mazoea kwa kuwa rais anataka kuona utumishi wenye ueledi ambao utaleta matokeo chanya ambayo yatatoa huduma chanya kwa wananchi.

“Mheshimiwa rais anafanyakazi kubwa kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao ili kusudi watoe huduma nzuri kwa wananchi kwahiyo niwaombe ninyi maafisa utumishi  kuwajibika vyema katika nafasi zenu acheni kuwa na roho mbaya,” amesema Kikwete.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, Butamo Ndalahwa amesema kuwa amepokea maelezo na atakwenda kuyafanyia kazi haraka na ameahidi kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kazi kubwa anayoifanya kwani Halmashauri ya Kibaha Vijijini inafaidika na utekelezaji wa miradi mikubwa  ya kimaendeleo kwasababu ya rais kupeleka fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles