29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Abel & Fernandes, St. Laurent wajitosa kuhamasisha watanzania kudhibiti kisukari

NA MWANDISHI WETU

Katika kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hususani kisukari, Kampuni ya Abel & Fernandes Communications, Quincewood Consulting pamoja na Kituo kinachotoa huduma za Kisukari  St. Laurent, imeungana na Serikali kudhibiti magonjwa hayo kwa kutoa huduma bure za upimaji na ushauri wa kitabibu kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam.

Pia, Watanzania wametakiwa kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara ili kudhibiti magonjwa hayo hususani ugonjwa wa kisukari ambao hadi sasa umeathiri zaidi ya watu milioni 1.5.

Wito huo umetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Abel & Fernandes, Fatma Fernandes  wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Kisukari duniani yaliyofanyika katika Kituo kinachotoa huduma za Kisukari  St. Laurent.

Maadhimisho hayo ambayo ambayo hufanyika kila ifikapo Novemba 14, yalienda sambamba na utoaji wa huduma za upimaji na ushauri wa kitabibu bure.

Katika maadhimisho hayo ya mwaka huu yalidhaminiwa na  Kampuni ya Abel & Fernandes Communications pamoja na Quincewood Consulting kupitia miradi yake ya  uwajibikaji kwa jamii.

Aidha, katika maadhimisho hayo, kampuni hizo zimeungana na Kituo cha Kisukari St. Laurent katika kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya Kisukari kwa kujenga uelewa kuhusu ugonjwa huo ambao kwa mujibuwa takwimu za wizara ya afya hadi sasa umeathiri zaidi ya watu milioni 1.5 nchini.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kisukari- St Laurent, Dk. Mary Maige alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya Kisukari duniani  kwa mwaka huu ni “Uuguzi na Kisukari”.

Alisema mwaka 2012 walifanya utafiti nchi nzima na kubaini kati ya watu 10, watu watano wana tatizo la kuchakata sukari mwilini hivyo kubaini kuwa asilimia 20 ya watanzania wana matatizo ya kuchakata kisukari.

“Kwa hiyo hili tatizo linazidi kuongeza, na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele tatizo linaendelea kuongezeka na tunatakiwa kuongeza juhudi zaidi ili kudhibiti tatizo hili ambalo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mtindo wetu wa maisha,” alisema.

Naye Katibu Mwenezi wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Johari Yusufu alisema kampeni hiyo ya mwaka huu inalenga kuwapa motisha wauguzi kutekeleza majukumu yao kwa uweledi ili kuwapatia huduma bora, stahiki na zenye staha wagonjwa wa kisukari nchini.

Alisema wauguzi wanahesabika kuwa nusu ya wafanyakazi wote wa sekta ya afya nchini. Ni kada mojawapo inayoweza kuwapatia huduma bora watu wanaoishi na magonjwa mbalimbali. Watu wanaoishi na Kisukari huhitaji zaidi msaada wa wauguzi katika kutibu tatizo hilo.

“Kwa hiyo tunawashauri wananchi wawe wanakwenda hospitali kucheki afya zao mara kwa mara,” alisema.

Aidha, Meneja uhusiano wa Kampuni ya Abel & Fernandes Communications, Abbas Jabir alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa pamoja wanaungana na wauguzi kuzuia na kutoa muongozo kuhusu Kisukari.

“Pia tunatoa huduma kwa mamia ya jamii kwa malengo ya kuwapatia taarifa muhimu kuhusu ugonjwa wa kisukari na namna ya kukabiliana nao.

“Maadhimisho ya mwaka huu ni muhimu kwetu wote kwani yanatoa fursa ya kupata huduma za afya bure kwa malengo ya kuboresha afya za watanzania wanaoishi na Kisukari, pia kuboresha maisha ya watu wanaoishi na ugonjwa huo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles