WAUMINI wa Kiislamu mkoani hapa wamemtaka Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir, kutomrudisha madarakani aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu kwa madai kuwa anachangia kurudisha nyuma maendeleo ya uislamu.
Sheikh Mustafa alisimamishwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kupisha uchunguzi ambako alidaiwa kutumia vibaya fedha, mali na ofisi za Baraza hilo.
Walikuwa wakizungumza mjini hapa jana kwenye kikao kilichofanyika kwenye Msikiti wa barabara ya tisa ambacho kiliongozwa na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Hamid Masoud Jongo, na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Selemani Lolila.
Walisema uongozi uliokuwa chini ya Sheikh Mustafa ulikuwa na matumizi mabaya ya fedha na mali hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya waumini wa dini ya kiislamu.
Mmoja wa waumini hao, Ramadhan Mzazi, alisema Mufti wa Tanzania anatakiwa kutomrudisha huku akieleza madai dhidi ya sheikh huyo kwamba akiwa madarakani alijimilikisha baadhi ya mali za BAKWATA jambo ambalo lilichangia kurudisha nyuma maendeleo.
“Sisi hapa Dodoma tuna shule mbili za Hijra na Jamhuri, shule hizi zimekuwa nyuma katika maendeleo sababu kubwa ni Sheikh huyo kuzitumia vibaya fedha zinazopatikana na walimu kila siku wanalalamika hawajapewa fedha sababu ikiwa ni yeye.
“Kwa manufaa ya Uislamu na maendeleo yetu Waislamu namuomba Mufti Sheikh Abubakari Zuberi, asimrejeshe madarakani kwani na sisi Waislamu tunataka maendeleo tumechoka kila siku sisi kuwa wa mwisho,” alidai Mzazi mbele ya viongozi hao wa BAKWATA.
Naye Awadh Mohammed alilitaka Baraza la Ulamaa kumpelekea taarifa kuwa Mkoa wa Dodoma hawamtaki Sheikh huyo kwa madai amekuwa na kiburi cha madaraka.
Akijibu hoja hizo, Mjumbe huyo wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Jongo, alisema ameyapokea malalamiko ya waumini wa kiislamu hivyo atampelekea Mufti Zuberi kwa ajili ya kufanya uamuzi kwa mujibu wa utaratibu.
“Mshenga hauawi, haya mliyoyasema nitampelekea Mufti, jibu lolote atakalokuja nalo mlikubali na msije mkanilaumu mimi manake mimi napeleka kile mlinielezea,’’ alisema Sheikh Jongo.
Wajumbe wa Bakwata kwa sasa wako katika ziara ya kutatua migogoro na matatizo katika mikoa mbalimbali. Mbali na Dodoma pia watazunguka katika mikoa ya Mwanza, Iringa, Njombe, Ruvuma na Morogoro.