31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Chenge ateuliwa kuwania uenyekiti wa Bunge

chengeNa Khamis Mkotya, Dodoma

KAMATI ya Uongozi ya Bunge  imepitisha majina matatu ya wabunge watakaowania nafasi ya uenyekiti wa Bunge.

Majina hayo yamepitishwa na kamati hiyo iliyoketi jana  kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana ikiongozwa na  Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho, zilisema  kikao kilikuwa na ajenda mbili  ambazo ni uteuzi wa majina ya wenyeviti wa Bunge  na kujadili ratiba ya Bunge.

Chanzo hicho cha kuaminika kililiarifu MTANZANIA kuwa waliopitishwa ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Mbunge mwingine wa Viti Maalumu, Najima Murtaza Giga wote kutoka CCM.

Chanzo hicho kilisema   wabunge hao wanakidhi matakwa ya kanuni inayoelekeza kuwa mwenyekiti wa Bunge ni lazima awe aidha mwenyekiti wa kamati au makamu mwenyekiti.

Katika uteuzi wa kamati uliofanyika mwishoni mwa wiki, Chenge ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, wakati Mwanjelwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Najima ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa mujibu chanzo hicho, majina hayo ambayo ni kati ya majina sita yanayotakiwa katika kanuni, yatawasilishwa katika kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Bunge utakaoanza kesho.

“Kanuni zinasema Spika atawasilisha bungeni majina sita  yapigiwe kura na baadaye yapatikane matatu, hawa ndiyo walioomba wamesimama wamejieleza na kamati imewapitisha.

“Hadi tunafanya uamuzi huu Ukawa walikuwa hawajaleta majina, sisi hatujui kama wataleta au hawaleti, lakini majina yaliyopitishwa leo (jana) ndiyo hayo,” kilisema chanzo hicho.

Mtanzania ilipotaka kujua iwapo Ukawa haitawasilisha majina mengine hali itakuwaje, wakati majina yaliyopo ni matatu na kanuni inasema ni zaidi ya matatu ili yapigiwe kura, chanzo hicho kilisema.

“Ni kweli kanuni zinasema hivyo, lakini sasa kama waliojitokeza ndiyo hao hao utafanyaje, utalazimisha watu wagombee?”

Kuhusu weledi na uwezo wa wabunge hao kumudu kiti cha Spika, chanzo hicho kilisema: “Mimi sina wasiwasi na hawa watu ni wazuri, Bunge wanalijua, mtu kama Chenge kwanza ni mwanasheria ana busara na hekima.

“Watu wasipime mambo kwa majina, kuna watu wengine wanafikiri katika hizi nafasi wangekuwapo akina fulani ndiyo waridhike hapana, usimhukumu mtu kabla hujampa nafasi.

“Kila zama na kitabu chake, hawa waliopitishwa tuwape nafasi tuwaone, tena wanaweza kufanya vizuri zaidi kuliko hao wengine waliopita,” kilisema chanzo hicho.

Mkuu wa Kitengo cha Bunge Habari, Elimu na Mawasiliano, Owen Mwandumbya   alikiri kumalizika kwa kikao hicho na kuahidi kutoa taarifa zake leo.

Bunge lililopita wenyeviti wa Bunge walikuwa ni Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Lediyana Mng’ong’o na aliyekuwa Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib.

Zungu amekosa fursa ya kutetea nafasi yake  kutokana na kukosa sifa na  hivi sasa yeye ni mjumbe wa kawaida wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba. Khatib na Mng’ong’o hawakufanikiwa kurejea bungeni.

Kamati ya Uongozi inaundwa na wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge, akiwamo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe  ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema).

Majina hayo yameteuliwa huku kukiwa na sintofahamu katika kambi ya upinzani bungeni kuhusu uteuzi na mpangilio wa wajumbe katika kamati mbalimbali za Bunge.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), havijaridhidhwa na uteuzi wa kamati hizo, hasa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinazopaswa kuongozwa na wapinzani.

Kutoridhishwa huko kumewafanya wabunge wa kambi hiyo kususa shughuli za kamati ikiwa ni pamoja na kutoshiriki uchaguzi wa wenyeviti wa kamati, jambo linaloleta taswira isiyoeleweka.

Tayari aliyekuwa Mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa   na Mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad wamewasili mjini hapa kwa ajili ya kukutana na wabunge wa Ukawa kwa majadiliano zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles