Asha Kigundula – Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, amesema kuwa, amekuwa akiumiza kichwa namna gani atatimiza matarajio ya viongozi na mashabiki wa klabu hiyo, ambao kiu yao ni kubeba taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Yanga imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo, baada ya taji hiyo kunyakuliwa na wapinzani wao wakuu Simba.
Akizungumza mara baada ya mchezo wao ya JKT Tanzania uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Mkapa na Yanga kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 Kaze alisema kuwa amefurahi kupata ushindi na kuendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo.
Kaze alisema kuwa, ni vigumu kuahidi moja kwa moja kuwa atatwaa taji hilo, lakini anapambana kuhakikisha anakata kiu ya wadau wa Yanga.
Kwa sasa watahakikisha wanapata ushindi katika kila mchezo wao ili kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Kaze aliwataja viongozi na mashabiki wa timu hiyo kuendelea kumpa sapoti ili kuhakikisha kwa pamoja wanafanikisha azma yao.
Kaze alisema bado wana kazi ya kufanya ili kuhakikisha hawapotezi mechi yoyote na kuendelea kuwaacha mbali wapinzani wao, ambao nao wana nafasi ya kuchukua ubingwa.
“Kushika kwetu nafasi ya kwanza ni dalili nzuri ya kutwaa ubingwa, mpaka sasa hatujapoteza mechi yoyote, tunahitaji kushinda mechi zetu ili tuweze kunyakuwa ubingwa, ambao sio kazi rahisi kutokana kila timu kuhitaji nafasi hiyo,”alisema Kaze.
Alisema kuwa, ushindani ni mkubwa , hivyo amekuwa akiwaza namna ya kufanya ili kufikia malengo.
Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 31, baada ya kushuka dimbani mara 13, ikishinda michezo tisa na sare nne.f