Na YOHANA PAUL-MWANZA
JUMUIYA ya Wajiolojia nchini (TGS), wamesema Rais Dk John Magufuli anastahili pongezi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika sekta ya madini nchini.
Hayo yalisemwa wiki hii na Rais wa TGS, Prof. Abdulakarim Mruma wakati wa uzinduzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa jumuiya hiyo ambapo alisisitiza mabadiliko hayo yamegusa wadau wote wa madini nchini ikiwemo wajiolojia, wachimbaji wadogo na wakubwa.
Prof. Mruma alisema mafanikio kwenye sekta ya madini yameonekana wazi kutokana na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa kutoka asilimia 3.3 mwaka 2011 na asilimia 3.5 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 5.2 kwa sasa.
Alisema TGS kwa kutumia taaluma zao wataendelea kumuunga mkono Dk. Magufuli kwa kuzingatia uongozi bora, maadili ya taaluma pamoja na kufanya kazi na tume ya madini ili mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa ufikie asilimia 10 kabla ya mwaka 2025.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli na gesi Tanzania (TPDC), Dk. James Mataragio alisema taasisi yake itaendelea kushirikiana nae TGS ili kufanyia utafiti maeneo tofauti yenye mafuta na gesi nchini ili kuifanya Tanzania kuwa kituo cha nishati Afrika Mashariki na kati.
DK. Mataragio alisema tayari TPDC wapo kwenye mchakato wa kukamilisha mradi wa kusambaza gesi majumbani na kwenye vituo vya kujazia magari ambapo mradi wa gesi unatarajiwa kujengwa Lindi kwani kadri uchumi unavyokua matumizi ya gesi yanaongezeka na hadi sasa jumla ya magari 500 yamethibitishwa kutumia gesi nchini.
Naye Mwakilishi kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Eric Kalondwa alisema wajiolojia ni watu muhimu sana katika sekta ya madini kwani bila wao huenda hata GGM isingekuwepo hivyo aliahidi kuendelea kuwapa ushirikiano TGS kwenye kila hatua.
Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliipongeza TGS kwa kazi kubwa inayoifanya ili kusaidia rasilimali za nchi kuendelea kuinufaisha jamii ya watanzania na kuwaomba kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili kazi zao ziwe zenye tija kwao na kwa taifa.