26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Kamanda Mtafungwa awaonya madereva

Na OSCAR ASSENGA-TANGA

KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Wilbrod Mtafungwa amewataka madereva  wanaoendesha mabasi na magari mengine ya abiria kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani hususani kipindi cha kuelekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka.

Mtafungwa aliyasema hayo jana Jijini Tanga wakati wa tukio la usalama barabara liliofanywa na Mabalozi wa Usalama Barabarani nchini (RSA) na kuwashirikisha wao wadau muhimu kwenye masuala ya usalama barabarani.

Zoezi hilo ni la uwekaji wa alama zisizofutika za kuvuka waenda kwa miguu na wengine ambapo vitu vyote vikiunganishwa vitasaidia kupunguza ajali.

 “Zoezi hili la kuweka alama zisizofutika za wavuka kwa miguu ni muhimu kwa waenda miguu na vitu vyote vikiunganishwa vitasaidia kupunguza ajali,mmefanya tukio muhimu kuzuia ajali na usimamizi mzima wa sheria za usalama barabarani,”alisema.

“Lakini pia niwakumbushe madereva wanaoendesha mabasi na magari mengine ya abiria kwenye kipindi cha sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya kuendelea kuzingatia sheria za usalama barabarani,”alisema.

Alisema mwendekosi, uendeshaji usingatia taratibu ni mambo ambayo tayari Jeshi la Polisi  wamekwisha kuweka mkakati wa kukabiliana nayo.

Alisema tayari kuna operesheni zimekwisha kupangwa kuhakikisha madereva wote wanaotumia barabara hizo wanafuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuheshimu alama lengo likiwa ni kuepusha ajali.

Tayari wakuu wa usalama barabarani nchini na makamanda wa Mkoa wamekwisha kuanza operesheni hizo.

Kwa upande Kamishna wa polisi kutoka makao makuu ya polisi Shabani Hiki alisema kundi kubwa la watu wanaoathirika na ajali za barabarani ni watembea kwa miguu na ndio maana wanaamua kuweka vivuko hivyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kwa kuweka vivuko madereva watazingatia na kufuata kanuni na taratibu za usalama barabarani kwa kupunguza mwendo kasi na kuwataka wananchi pindi wanapoona vivuko hivyo kuwa ndio mahala sahihi kwa wao kuvukia barabara tofauti na maeneo mengine ambayo yanahatarisha maisha yao.

Naye Mwenyekiti wa taasisi ya mabalozi (RSA)Tanzania John Seka alisema kama sehemu ya mkakati wao Tanzania watahakikisha wanashirikiana na Jeshi la Polisi kuendeleza elimu ya usalama barabarani kwa nia ya kuhakikisha wanatokomeza au kupunguza ajali za barabarani.

Alisema Tanzania kama Nchi imejiwekea malengo ya kwamba itakapofika mwaka 2030 ajali za barabarani zinapaswa kupungua na kuwa chini ya asilimia 50 zinazotokea hivi sasa.

‘’Hilo ni lengo ambalo imejiwekea na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kwa kushirikiana na idara na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau kutoka sekta binafsi bado wana dhamira ya kuhakikisha lengo hilo linatimia na lilipangwa kutimia 2020,”.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu na utafiti unaoendelea vipo viashiria kwamba malengo ya kupunguza ajali kwa asilimia 50 ifikapo 2020 hayatatimia sababu mwaka unakwenda kukamilika kabla ya lengo.

Aidha alisema kidunia umoja wa mataifa ulitambua hilo ya kwamba inawezekana ifikapo mwaka 2020 mwishoni lengo la kupunguza ajali za barabarani litakuwa halijatimia kwa kupitia malengo ya millennia endelevu umoja wa mataifa uliongeza miaka mingine 10 katika malengo ya kidunia ambapo kila nchi inatakiwa ifikapo 2030 nchi zote ziwe zimepunguza ajali kwa asilimia 50.

Sambamba na hayo mwenyekiti huyo alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ajali zinazotokana na masuala ya barabarani kwa sasa duniani zinaua watu 1,350,000 lakini kati ya hao pia inaacha majeruhi kati ya milioni 40 hadi 70 kila mwaka.

‘’Tunaposema kupunguza ajali kwa asilimia 50 ina maana ya kwamba ile 1,350,000 ya vifo ipingue nusu na siyo kazi ndogo kwasababau ya changamoto zilizopo tunaposema ajali zinapungua, magari yanaongezeka, shughuli za kibinadamu zinaongezeka lakini ukiacha shughuli za kibinadamu watu wengi sasa wanahamia mijini na vyombo vya usafiri vinabadilika,’’alibainisha Seka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles