26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

SADC-Troika, UN kuboresha mfumo wa usalama ndani ya DRC

Na NELSON KESSY -GABORONE, BOTSWANA 

ASASI ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) zimekubaliana kuboresha mfumo utakao weka ulinzi bora na usalama ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akithibitisha kuhusu mashirikiano ya mfumo wa kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amemuwakilisha Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli katika mkutano huo amesema kuwa kamati ya utatu inayoshughulika na usalama ndani ya jumuiya ya SADC imekutana kwa dharura ili kuweza kuangalia namna ya kukabiliana na matishio ya ugaidi yanayotishia sana hali ya amani na usalama katika nchi zilizopo ukanda wa SADC ikiwemo Msumbiji, Congo DRC na Tanzania.

Mkutano huo wa Dharura wa Wakuu wa Nchi wa Utatu wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, nchi zinazochangia Vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Msumbiji  ulifanyika juzi Novemba 27,Novemba 2020 mjini Gaborone, Botswana ambapo pamoja na mambo mengine umeangalia masuala mbalimbali yanayohusu amani, ulinzi na Usalama ndani ya SADC.

“Tumeangalia kwa undani mapendekezo mapya ya mfumo wa ulinzi katika enao la DRC ambapo nchi tatu zinazoshiriki katika kuimarisha Ulinzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo nchi tatu zinashiriki kuimarisha ulinzi na usalama nchini DRC (Tanzania, Malawi na Afrika Kusini) kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zitaendelea kuimarisha masuala ya amani, Ulinzi na usalama Nchini DRC kwa kutumia mfumo mpya utakao weka ulinzi bora na amani nchini DRC,” amesema Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza kuwa, kupitia mkutano huo pia limejadiliwa suala la hali halisi ya usalama ndani ya nchi wanachama ndani ya SADC na kuona jinsi ya kutumia usalama wetu kwa ajili ya kujenga uchumi wa ukanda wetu wa kusini mwa Afrika

Kwa upande wake Rais wa Botswana, Dk. Mokgweetsi Masisi ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo amezipongeza nchi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Visiwa vya Shelisheli kwa kufanya chaguzi ambazo zilikuwa huru, haki na amani na kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano huo wa kuwa na demokrisia ya uhuru, amani na haki.

“Matokeo ya chaguzi hizo ni mfano mzuri kwetu sisi kama nchi wanachama wa SADC kujifunza mfano kutoka kwa wenzetu,” Amesema Dk. Masisi.

Dk. Masisi ameongeza kuwa pamoja kufanya chaguzi huru haki na za amani, kuna mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa SADC kama vile, ugaidi, uhalifu wa kimtandao na vikundi vya waasi jambo ambalo limepelekea wakuu wan chi na serikali kukutana Botswana na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa siyo za nchi moja moja bali na kuzitaka nchi zote kuungana na kukabiliana na vikundi hivyo vya kigaidi.

“Mtakumbuka kuwa katika mkutano wetu wa SADC uliofanyika mwezi wa nane mwaka huu tulitoa ripoti iliyoonesha kuwa na baadhi ya ugaidi kwa baadhi ya nchi zetu za SADC, pamoja na ripoti kuonyesha kuwa kuna hali ambayo siyo shwari kwa baadhi ya nchi wananchama, kuna haja ya kuungana pamoja na kuhakikisha kuwa vikundi hivi vya kigaidi vinatokomezwa katika ukanda wetu wa SADC,” Amesema Dk. Masisi.

“Ni jukumu letu sote kuipa ushirikiano Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo hasa upande wa Mashariki mwa DRC na kuhakikisha kuwa amani ya nchi hiyo inalindwa kwa kutokomezwa kwa vikundi vya kigaidi vinavyochangia kutoweka kwa amani nchini humo, na ndiyo maana leo tumekutana hapa ili tuweze kuona na jinsi gani ya kumsaidia mwenzetu DRC,” aliongeza Dk. Masisi

Pamoja na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama  inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.

Ni mara ya kwanza kwa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC – TROIKA) kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (Covid-19).

Mkutano huo ulihudhuriwa na, Rais wa Botswana Dk. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Rais wa Malawi Lazarus Chikwera, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi, Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Msumbiji Jaime Neto aliyemuwakilisha Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles