Na AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM
UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu(NIMR) umebaini kuwa wagonjwa wenye Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanaotumia dawa wako hatari kupata ugonjwa wa kisukari.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum, Mtafiti kutoka Taasisi hiyo, Dk. Jeremia Kidole alisema utafiti huo ulihusisha watu ambao hawana virusi vya Ukimwi 655 na ambao wanavirusi vya Ukimwi wanaotumia dawa 656.
“Huu ni utafiti ambao tulikuwa tunaangalia ukubwa wa tatizo la kisukari katika wagonjwa ambao hawana virusi vya Ukimwi(HIV) na wale walivyonavyo lakini hawatumii dawa na wale wenye HIV ambao wanatumia dawa.
“Utafiti ulibaini kwamba wagonjwa ambao wana HIV na wanatumia dawa wako katika hatari ya kupata kisukari na wagonjwa ambao hawana HIV na hawatumii dawa wanahatari ndogo ya kupata kisukari.
“Tafiti hii imefanyika katika Mkoa wa Mwanza na imehusisha wagonjwa waliofuatiliwa kwa kipindi cha miaka 10 ni wagonjwa ambao alichukuliwa mwaka 2005 mpaka 2009 na tukaja kuwaona tena mwaka 2017 hadi 2022,”alieleza Dk Kidole.
Aliongeza; “Hofu yetu ni kwamba hawa wagonjwa ambao wana HIV na wako kwenye dawa wengi wao wanapata magonjwa ya kisukari na magonjwa mengi yasiyoambukiza.
Dk. Kidole alisema hali hiyo hufanya matibabu kuwa mzigo kwa mgonjwa kutumia dawa kutokana na magonjwa hayo kuwa ya muda mrefu.
Dk. Kidole alibainisha kuwa katika utafiti huo walibaini kuwa ufanyaji mazoezi kwa wanaotumia dawa za VVU hupunguza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari.
“Tukajaribu kuangalia ni vitu gani ambavyo tunatakiwa kufanya ili kupunguza tatizo cha kwanza tukagundua kuwa wale ambao ni HIV na wako kwenye dawa na wanafanya mazoezi hatari yao ya kupata magonjwa ya kisukari inapungua.
“Katika kufanya hayo tukaamua kushauri serikali iweze kuingiza ‘component’ ya mazoezi kama mojawapo ya matibabu ya HIV na kisukari kwa wagonjwa kwasababu mazoezi ni kitu muhimu sana na kama itakuwa sehemu ya matibabu kwa wagonjwa hao itasaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza,”alieleza Dk Kidole.
Pamoja na hayo alisema bado wanaendelea kufanya utafiti ili kubaini chanzo cha tatizo hilo kama dawa hizo zinasababisha tatizo au virusi ndio sababu.
“Kwa sababu tunaelewa upataji ugonjwa wa kisukari unahusishwa na kongosho kutokufanya kazi vizuri ambalo linatoa vichocheo vya kupunguza kisukari sasa vile vichocheo visipotoka vya kutosha au vinaweza kutoka vya kutosha na vikashindwa kuunguza sukari au isitoke kabisa .
“Sasa tunataka kubaini kama vinatoka na havina nguvu tatizo ni nini ?na kama havitoki tatizo ni nini? Kwahiyo katika utafiti wetu wa awamu ya pili tutaliangalia hilo,”alifafanua Dk Kidole.
Aliogeza; “Kingine tunachofikiria ni kwamba tunataka kuangalia kama ARVs ukitumia zinaongeza mafuta sehemu za tumbo na ukiwa na kitambi ni hatari ya kupata kisukari lakini pia HIV yenyewe inaweza kwenda kwenye kongosho na kufanya vitu ambavyo vinabadilisha ule mfumo wa utengenezaji wa insulin.