Mwandishi wetu, Dar es salaam
FOMU za kuwania nafasi mbali mbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo nafasi ya Spika na naibu wake zimeanza kutolewa jana na leo, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni.
Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ilisema wenye sifa stahiki kwa mujibu wa sheria na wanaoomba wafikiriwe na chama kwa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Naibu Spika, Meya wa Halmashauri ya Jiji au Manispaa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya wajitokeze kuchukua fomu hizo.
Taarifa hiyo ya Polepole ilieleza jana kuwa Sambamba na sifa stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi, waombaji wote lazima wawe wanakidhi sifa za uongozi kwa mujibu wa wa katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 200 ikisomwa pamoja na kanuni ya maadili na uongozi toleo la mwaka 2017.
“Kwa nafasi za spika na naibu spika wa Bunge, fomu zinapatikana katika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, Ofisi ndogo ya Makao Makuu, Lumumba jijini Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar,” alisema.
Alisema kwa nafasi ya Meya wa Jiji au Manispaa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya fomu zinapatikana katika ofisi za CCM za Wilaya.
“Tarehe rasmi ya kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi zote tajwa hapo juu ni jana Novemba 2 na leo Novemba 3 saa 10 jioni,” alisema Polepole.
Aidha alisema taarifa iliyotolewa izingatiwe na vikao vya uongozi na uamuzi ngazi ya mkoa na wilaya kwamba Novemba 4, 2020 ziketi Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya na kutoa mapendekezo na Novemba 5 ziketi Kamati za siasa za Halmashauri Kuu za CCM Mkoa na kutoa mapendekezo.
Alisema mapendekezo ya Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa yawe yamefika ofisini kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma si zaidi ya saa 10 jioni Novemba 6, 2020
“Niwatakie kila la kheri katika kujitafakari, kujitathmini na kumtanguliza Mungu mbele kwa wale watakao omba kufikiriwa na Chama kwa dhamana tajwa, nitawakie utekelezaji wa haraka wa taarifa hii na maelekezo yaliyomo ndani yake,” alisema Polepole.