Derick Milton, Simiyu
MKUU wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu Benson Kilangi amewataka wazazi, walezi kujenga tabia ya kulinda watoto wao wenyewe dhidi ya magonjwa ya mlipuko yakiwemo minyoo na kichocho.
Kilangi amesema kuwa jamii haina budi kubailika na kuacha tabia ya kuisubiri serikali au wadau wa afya katika kuhakikisha afya za watoto wao zinakuwa salama dhidi ya magonjwa hayo.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema hayo jana wakati akizungumzia kampeni ya kutoa vidonge vya minyoo na kichocho kwa watoto wadogo ambalo linatarajiwa kufanyika katika Wilaya yake.
Alisema kuwa jamii inayo uwezo wa kuhakikisha watoto wake wanakuwa salama, kwani magonjwa mengi ya mlipuko yanaweza kuzuirika ikiwa wazazi au walezi watazingatia usafi.
“ Magonjwa ya Minyoo na kichocho yanatokana na uchafu, endapo jamii itaweka kipaumbele kuhakikisha inazingatia usafi, itahakikisha inawalinda watoto, itakuwa imepunguzia serikali mzigo wa kuwalinda,” alisema Kilangi.