NA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete, anatarajiwa kutunukiwa shahada ya heshima cha uongozi kutoka Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (OUT) kwenye mahafali ya 30 chuoni hapo leo.
Mbali na Kikwete pia Rais wa awamu ya 15 kutoka Chuo Kikuu cha Korea ya Kusini, Profesa Chae – Hong Suh pia atatunukiwa shahada ya heshima kwa mchango wake mkubwa wa kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika kwa kutumia teknolojia ya sayansi.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda alisema Rais Kikwete alipokuwa madarakani aliweza kusuluhisha migogoro mbalimbali ukiwamo uliotokea Kenya baada ya uchaguzi 2007.
“Mkuu wa chuo hiki leo atawatunuku viongozi hao pamoja na wengine ambao jumla watakuwa 69 katika fani mbalimbali,” alisema Bisanda.
Profesa Bisanda alisema Kikwete alipokuwa madarakani aliweza kukuza na kuimarisha uchumi wa Tanzania na kutembelewa na marais wa dunia hivyo ana kila sababu ya kupewa cheti hicho.
Katika mahafali hayo wahitimu watatu watatunukiwa Shahada ya Pili ya Uzamivu (PHD), wahitimu 20 watatunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani za uchumi na elimu na wengine 22 watatunukiwa shahada ya kwanza wakati Stashahada watakuwa 15 na Astashahada watakuwa sita.
Bisanda alisema chuo hicho kimeweza kufungua matawi kila mkoa lakini na ni chuo pekee nchini chenye wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kupitia masafa marefu kwa kutumia Tehama.
Alisema katika mahafali yaliyopita zaidi ya wanafunzi 26 kutoka mataifa mbalimbali walitunukiwa vyeti.